Taabu

120 14 6
                                    

Hawa, msichana mwenye umri wa miaka kumi na mmoja alibaki peke yake  darasani kwenye kiti chake. Alikuwa amezongwa na mawazo tele. Machozi yalikuwa bado hayajakauka shavuni. Macho yake mekundu yalijawa na hawafu. Mikono na miguu yake ilitetemeka kama vile ya mraibu aliyekosa funda.

Kwenye dawati lake ilikuwa daftari ya kiingereza. Maswali waliyoachiwa kama kazi ya ziada, hakuweza kuyajibu na yale machache aliyajaribu, mwalimu alitia alama kubwa za makasi na kumvamia kwa hamaki.

Kengele ilipolia, wanafunzi walikimbilia darasani wasiipate adhabu. Mlangoni ungewaona wamebanana kama ndizi kila mmoja aking'ang'ana kuwa ndani ya darasa kabla ya adhabu kumfikia.

Kengele ile ilimpa kiwewe Hawa. Sio kuwa alichelea adhabu ya 'kuasi kengele' lakini ya kuwa mjinga. Somo lililokuwa baada ya mapumziko lilikuwa hisabati. Sio kama hajakamilisha kazi ya ziada, ila anajua tu majibu yake hapajatokea hata siku moja yakawa sahihi.
Pia kuna ile seti... Bado hajasahau kichapo alichopata kutoka kwa babake, simba mkali, kwa sababu bado mgongo wake na makalio yake yanawashawasha.

"Mister Kaya, mister Kaya" wanafunzi walinong'ona walipomwona mwalimu akijongea. Kimya cha kishindo kilitua darasani jambo ambalo lilizidisha mdundo wa moyo wake Hawa.

Alipofungua mlango, wote walisimama kidete na kumwamkua. "Good morning mister Kaya!"

Mwalimu aliingia na madaftari na mfereji mweusi wa mpira almaarufu 'cheusi' pale shuleni. Alivitua vitabu vile mezani na kuwaamuru waketi. Awamu ya kwanza ikang'oa nanga.

"Hawa Maimuna." aliita mwalimu ilipotimia zamu yake. Hawa aliitika kwa sauti nyonge na kusongelea mezani. "Sufuri! Yaani hukupata hata moja. Ng'o?" alibweka mwalimu. "Baradhuli wewe! Unadhani hapa ni holiday camp?" mwalimu alimvamia kwa mijeredi na matusi. Masikini Hawa!

Kilichomuuma Hawa zaidi ni kuwa wanafunzi wenzake waliokuwa wamepita walimcheka jinsi alirukaruka na kulia kwa uchungu. Naye mwalimu, kana mwwmba alijua, alihakikisha mijeledi imempata alipokuwa anauguza kichapo cha babake. Uchungu aliouona ulimfanya aitamani jumapili kwani ndiyo siku pekee asiyoona adhabu.

Machozi yalimtoka hata yakaisha akabaki anapiga unyende tu. Nao unyende huo ulijulikana na wote. Waalimu na wanafunzi pia. Hakuna asiyesikia sauti ile siku baada ya siku.

Alipokuwa anarukaruka pale mbele ya darasa, alihisi kiowevu fulani chenye joto kikiteremka miguuni na kuingia kwenye kiatu chake.

"Unajikojolea ee?" alihitimisha adhabu mwalimu. "Nenda ulete maji haraka!"

Hata alipokuwa nje ya darasa, aliusikia mngurumo wa vicheko vya wanafunzi wale wa darasa lake.

Hawa aliona aibu kuu siku ile. Yeye alikuwa mwenye umri mkubwa kuliko wanafunzi wengine wote wa darasa la nne. Hili lilitokana na uamuzi wa waalimu na wazazi wake kuwa alirudie darasa hilo kwa kuwa hakupita mitihani yake.

Jioni ilipofika, wanafunzi walikimbia nyumbani kwa furaha lakini Hawa alitembea polepole akifikiria vipi atamweleza baba yake. Mazoezi ya ziada walikuwa wamelimbikiziwa kama punda na nina yake alitarajia kuipata nyumba shwari atokapo sokoni.

"Umechelewa wapi? Saa ngapi hii?" Mama yake alimuamkua kwa makofi. Ilikuwa saa kumi na moja kasorobo. Kachelewa kwa robo saa kulingana na mamake.

Mama yake alienda nje kushona vitambaa akamwacha bintiye wa pekee aishughulikie maskani. Naye Hawa alijikaza akapiga deki, akang'arisha vyombo na kupika chajio.

Alipofika baba yake, alimwita kwa hasira. "Amenitajia nini mama yako? Hivyo sasa umeanza kuchelewa?" kichapo kilichofuata afadhali ninyamaze. "Seti yako nitainunua kesho." Alisema akipumzika kitini. Jasho linampita utosini kwa kazi aliyoifanya - kuwadhibu bintiye eti.

Maskini Hawa alifululiza chumbani mwake kwa kwikwi. Aliona heri dunia immeze hai yasimpate yaliyomuandama. Si nyumbani. Si shuleni. Alichokiona ni kimoja tu. Adhabu ya kosa asilojua.

Usiku huo, Maimuna alipanga njama kabambe. Uamuzi huo ungehitimisha mateso aliyoyapitia. Kidosho huyu aliamua kutoroka nyumbani. Alipanga kutoroka asubuhi wakati anaelekea shuleni. Angemwemdea amu yake aliyeishi mbali hata kama kwa miguu. Aliamini palipo nia pana njia

Chozi NyongeWhere stories live. Discover now