Episode 3

44 2 0
                                    

Inaendelea….
*    *     *

Bwana Mtanzi Matambo alikuwa mgombea mwenza wake Bwana Tadi. Alikuwa ameketi sebuleni mwake akitazama mkutano wa Tadi. Alinyanyuka pindi mkutano ule ulipoisha na kumpigia Mhazili simu.Sasa alijua ni  wapi pa kumshindia Tadi.
Mtanzi alikuwa ‘kijana’ kama alivyojiita na alisema kuwa wakati wa wazee umeisha. Aliwakusanya wandani wake na kuelekea uwanja wa Takia. Msafara wake, kama ilivyokuwa ada, uliandamwa na wafuasi wake toka nyumbani hadi uwanjani. Watu waliposikia tu kipaza sauti walivaa pochi nambari mguu nielekeze hadi uwanjani.
“Mjuavyo, hizi ni nyakati za kidijitali. Wazee ni analogi. Sisi kama vijana tuna nguvu, upevu wa akili na vile vile macho ya kuona vizuri. Wazee wasioona vizuri wanatuambia nini? Kuna haja gani kutegemea mshumaa unaojua kuwa utayeyuka na kuzima wakati wowote?
“Mimi kama Mtanzi sitetereki kamwe. Najua fika kuwa mwamko mpya huletwa na vijana wala si Wazee.”
Umati haukusita kushangilia maneno ya Mtanzi. Alitia bashasha usoni. Alitazama hadhira yake namna ulivyotulia kumsikiza.
“Katika kampeni yangu ninatambua mchango wenu kama wanamji na wenyemji. Hivyo…!” Alisema akiashiria Mhazili autoe mkoba uliokuwa kando yake.
“Mkoba huu una pesa ambazo ni zenu; mnunue mahitaji yenu. Ni kionjo tu. Wajua tena, ‘mtegemea nundu haachi kunona.’ Mkitupa kazi basi pesa hizi zitaongezeka maradufu.”
“Huree!” Umati ulishangilia huku foleni ikipigwa.
“Mkinipa kura mtapata mapato zaidi ya hii. Hii ni ishara tu ya mengi mazuri ambayo yatakuja. Mtaanza kuwa matajiri. Gharama ya maisha itashuka. Karo ya shule itapungua na mengi mazuri yatafuatia. Hamna haja kwangu kunena mengi kwani tukiahidi tunatimiza. Wale wanaodai kuwa na tajriba nawakumbusha kuwa wakati wa Wazee uliisha. Waende wakapumzike nasi tutawatengei pensheni ya kijikimu.” Umati ulimshangilia kwa jazba Sasa sababu kila mmoja alitia mfukoni shilingi hamsini.
Waliokosa migao yao walirudi wakinungunika na kukashifu Mtanzi. “Vipi anatoa pesa kidogo ilhali pesa anazo nyingi?” Alisikika kidosho mmoja akisaili. “Nakwambia kura yangu hapati!” Alizidi kulalamika.
“Hasaa! Yeye mwenyewe amesema pesa kwetu, kura kwake!” Aliongezea mwenzi wake.
“Na pasipo pesa hapana kura.” Alicheka kidosho yule.

Itaendelea…..

VUTA N'KUVUTE Où les histoires vivent. Découvrez maintenant