PART ONE: USHUHUDA, UNABII NA JUMBE MAHSUSI KWA KANISA LA JIONI

15 0 0
                                    

Dibaji

Ushuhuda wa maisha ya wokovu na huduma tangu kumjua Yesu (1987 hadi sasa).

By Pastor Nestory Ihano

Ndugu mpendwa msomaji, nakusalimu kwa jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai. Kwa muhtasari, niliokolewa na Yesu nikiwa darasa la nne mwaka 1987 mwezi wa kwanza katika kijiji cha Nyamilama wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza, na kuwa mshirika katika dhehebu linalojulikana leo kama The Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT). Mwaka 1989 jioni moja nikiwa njiani kuelekea nyumbani, nilipokaribia kabisa na nyumbani, nalikuwa katika hali ya utulivu ambapo ghafla nalisikia uwepo wa Mungu unanizunguka na nikajikuta natokwa na machozi bila kujua cha kufanya, baadaye nilisikia sauti ya Mungu moyoni mwangu ikisema nami maneno “utakuwa mwinjilisti”. Kabla ya siku hiyo, nilikuwa ninasikia mzigo mzito ndani ya moyo wangu, hali ambayo ilikuwa ikinifanya nijikute ninabubujikwa na machozi hata kama niko katikati ya watu. Ilitokea hivyo mara nyingi tangu niokoke, siku zingine kaka yangu Rev. Elias Simon, ambaye ndiye alikuwa mchungaji katika kanisa letu alikuwa akigundua hiyo hali, ananichukua tunaenda mbali na eneo la nyumbani ananiombea.
Mwaka 1991 nikaanza masomo ya sekondari katika seminari ya Makoko - Musoma, lakini mwaka 1993 kukawa na tatizo la ada lililoambatana na kufukuzwa kwangu pamoja na wenzangu wengi kutoka shule, hivyo nikasimama masomo kwa muda wa miaka miwili. Nikiwa seminari ya, maisha yangu kiroho hayakuwa mazuri kwa sababu nilijikuta nimejiunga na makundi mabaya baada ya kuingia kidato cha pili ambapo ilinisababishia kujifunza utumiaji wa vileo (k.v. sigara); kitu ambacho kilikuwa hakiruhusiwi pale seminarini. Kwa ujumla maadili ya wanafunzi wote yalishuka sana pale seminarini kila iitwapo leo, ndipo uongozi wa jimbo la Katoliki Musoma uliamua kuwa wanafunzi na waalimu wote wasimamishwe masomo na kazi kwa muda halafu waitwe upya lakini kwa kuandika barua ya maombi ya kurudi seminarini. Tuliandika upya maombi ya kurudi seminarini lakini watu wengi sana hawakurudishwa nikiwemo na mimi. Licha ya kutokurudishwa masomoni, kwa mwaka huo sikuwa na ada ya kulipa na ukizingatia ada ilipanda mara mbili na nusu mwaka huo. Matatizo haya mawili yakapelekea mimi kusimama masomo. Ilipofika Juni 1993, niliamua kwa dhati kutengeneza uhusiano wangu na Mungu na kurudi tena katika wokovu hasa baada ya mfululizo wa matukio mbalimbali ambayo Mungu aliyatumia kuzungumza na mimi kumrudia yeye. Mojawapo ilikuwa ni pale ambapo nilianza kuachwa na wasichana niliokuwa na mahusiano nao kimapenzi kwa sababu katika wote hao hakuna hata mmoja ambaye tulifanikiwa kujuana kimwili ambapo niliona wazi kabisa kuwa Mungu hakutaka mimi nishiriki ngono kabla ya ndoa. Tukio lingine ni pale siku moja nilipovuta sigara kifua kikanibana sana jambo lililosababisha niamue kuacha sigara; lakini pia shuhuda nilizosikia zikisimuliwa pale nyumbani za mambo ya siku za mwisho na mengine mengi ambapo kupitia hayo nilisikia kama Mungu anasema na mimi hatimaye niliamua kuachana na maisha ya giza kwa nguvu nyingine tena.
Naweza kusema sababu iliyosababisha kurudi nyuma ilikuwa ukosefu wa mafundisho sahihi kanisani yanayomlenga kijana anayetoka utoto kuelekea ujana (adolescence to youth). Ndiyo maana baada ya kumrudia Yesu, nilipata mzigo mkubwa sana wa kusaidia vijana wenzangu katika maisha ya ujana na changamoto zake. Baada ya kumrudia Yesu hiyo 1993 nikiwa nipo tu nyumbani masomo nimesimama, Mungu alinipitisha katika maisha ambayo sikuelewa kwa wakati huo kusudi lake lilikuwa nini. Kwa miaka hiyo miwili nikaishi maisha yenye mapito mengi ambayo yalikuwa ni shule ya Mungu kunifundisha mambo mengi. Nilijaribu kutafuta ada ya shule kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile kuvuta kokoro, kuvua sato (Nile perch), biashara ndogo ndogo za aina nyingi, ushonaji wa nguo, lakini hakukuwa na mafanikio yoyote maana miaka hiyo 1993 na 1994 iliambatana na tatizo la njaa. Msemo wa waswahili usemao ’ng’ombe wa maskini hazai’ niliuona ukitenda kazi kwa dhahiri maana hata kile kidogo nilichokuwa nakipata kwenye biashara ilibidi kipambane na adui njaa katika familia niliyokuwa naishi. Kwa kipindi hicho cha miaka miwili nikiwa na mlezi wangu kihuduma Rev. Daudi Jinega, nilijifunza kwa uhalisia maisha ya huduma na mambo mengi yanayoelekeana na huduma pamoja na kanisa kwa ujumla. Hiki ndicho kipindi nilipojifunza hata kuhubiri na kati ya 1994 hadi 1996, nilifanya mikutano ya hadhara mingi na hata mikutano ya uamsho makanisani katika wilaya ya Kwimba na Magu; na Mungu alikuwa akionekana. Katika muda huo Mungu aliweka mzigo mkubwa sana ndani yangu juu ya kanisa. Mungu aliendelea kunifundisha kwa njia ya Roho Mtakatifu kuhusu kanisa kwa kiasi chake. Nilijikuta katika maisha ya maombi yangu nikiombea kanisa kwa muda mrefu sana. Ndani yangu kulikuwa na shauku ya kutaka kuona katika kanisa la Mungu, nguvu ya Mungu ikionekana kwa uwazi kabisa na Mungu atembee pamoja na kanisa lake. Maombi ya aina mbalimbali yalifanyika kwa ajili ya kuitikia hali hii niliyokuwa nikiisikia ndani yangu kwa ajili ya kanisa. Si rahisi kuandika kila kitu hapa.
Mwaka 1995, niliweza kupata nafasi ya kuendelea na masomo tena ikiambatana na kuongoza kanisa la pale kijijini kwa muda wa miezi tisa; wakati huo nikiwa ninasoma sekondari kidato cha tatu baada ya kurud shule tangu niliposimama tangu 1993. Nilimwona Mungu akitenda mambo makubwa pamoja na kuwa nilikuwa bado mdogo kiumri. Kanisa liliongezeka sana na si hivyo tu, Mungu alikuwa akitembea ndani ya kanisa akifungua watu wenye shida kwa kiasi kikubwa sana. Si rahisi kuongelea shuhuda hizo hapa.
Mwaka 1996 Mungu alisema nami mara ya pili kuhusu wito ambao niliusikia mwaka 1989. Ilikuwa wiki ya mikutano ya Injili ya Mwinjilisti wa kimataifa Reinhard Bonnke kutoka Frankfurt Ujerumani, mikutano iliyofanyika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza ambapo tukiwa kwenye semina ya asubuhi kwenye ngazi za kupanda kuingia ukumbi wa Shinyanga Guest (maana nilikosa nafasi ukumbini palijaa mapema), nilisikia sauti ya Mungu moyoni mwangu ikirudia kusema nami. Sauti hii safari hii ilikuja kwa nguvu kabisa na maneno ya kuwa, “nimekuita uwe mtumishi wangu”. Nililia sana mbele ya uwepo mkuu wa Mungu. Baada ya mwaka 1996, Mungu aliendelea kuwa pamoja nami katika huduma. Hata nilipoendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita (1997 – 1999) katika shule ya Musoma High School, niliendelea kumwona Mungu katika huduma ya uimbaji na kuhubiri hata huko shuleni. Mwaka 1997, nilipokuwa natafakari juu ya hali ya kanisa, nilianza kuona picha za makongamano ya uamsho yakifanyika katika mawazo yangu na yalikuwa yakigusa sana moyo wangu. Mwaka 2000 mwezi wa nane Mungu alinifanikisha kupata mwenzi wa maisha aitwaye Stela Leonard, jambo ambalo nalo lilikuwa na mapito ya aina yake.
Mwaka 2001 nilijiunga na masomo ya chuo kikuu. Kwa kipindi kati ya 1999 na 2003 nilipita katika wakati wa ukimya fulani ambapo sikuwa nasikia Mungu akisema nami neno lolote hadi ilipofika mwaka 2003 ambapo Mungu alianza kusema nami kwa nguvu kabisa juu ya kanisa. Lakini Mungu kwa kipindi cha ukimya huo aliinua huduma ya uimbaji kwa kiwango kingine kabisa japo tangu 1988 nilikuwa nikifanya huduma hiyo. Kipindi hiki ikabidi tena kuanza maombi kwa ajili ya kuombea kanisa, maana ndilo hitaji ambalo lilikuwa limejaa moyoni mwangu. Kwa wakati huo huo mwaka 2004 nikiwa bado nasoma chuo kikuu, Mungu akanifanikisha kurekodi album ya kwanza ya nyimbo inayoitwa ”Yesu ni mwema”. Mwaka 2005 Juni nikamaliza masomo na kutunukiwa shahada ya ualimu (BA. Education).
Mwaka 2004 baada ya kukaa na mzigo juu ya kanisa kwa miaka hiyo michache, Mungu alianza kuzungumza nami tena kwa habari ya kanisa kwa hatua nyingine tena.  Tangu Mungu aliposema nami kuhusu kanisa alianza kunifundisha jinsi kanisa lake anavyotarajia lionekane, nguvu anazotarajia zionekane na kadhalika. Somo hilo lilieleweka kwangu kabisa. Tangu wakati huo nimekuwa katika kujiuliza sana kwa nini Mungu alikuwa ananifundisha habari ya Kanisa lake kwa uzito sana. Nimeendelea katika maombi kwa ajili ya kanisa nikijaribu kuwashirikisha na watu wengine ambapo nikagundua kwamba wengine hawaoni hali ya kanisa kama ninavyoona mimi. Wakati mwingine niliweza hata kujishitukia kuwa labda mimi nitakuwa na matatizo yangu binafsi nikiangalia walio wengi hawaoni kama ninavyoona mimi. Lakini nikawa nashangaa muda unapofika wa Mungu kusema nami, mpaka naamini kuwa ni yeye ndiye anayesema nami juu ya kanisa. Nimekuwa na machozi mengi sana juu ya kanisa nikikumbuka ambavyo Mungu amekuwa akisema nami juu ya kanisa lake hasa kwa nyakati hizi. Maana mambo mengine ambayo Mungu amekuwa akizungumza ni madhaifu yaliyoko katika kanisa la Mungu leo.

You've reached the end of published parts.

⏰ Last updated: Jul 16, 2020 ⏰

Add this story to your Library to get notified about new parts!

Five mistakes of the Church Where stories live. Discover now