Aina za Vielezi
Vielezi vya Mahali
Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.
k.m: nyumbani, kazini, shuleni
Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya Wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika
k.m: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi
Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
Kisaka na Musa watakutana kesho
Vielezi vya Idadi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi
a) Idadi Kamili
Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika.
k.m: mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
b) Idadi Isiyodhihirika
Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili
k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
Yeye hunipigia simu mara kwa mara
VIelezi Vya Namna
Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:
a) Vielezi vya Namna Halisi
Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine).
k.m: vizuri, ovyo, haraka
Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
Mama alipika chakula upesi
Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela
b) Vielezi vya Namna Hali
Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo
k.m: kwa furaha, kwa makini,
Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
Mtoto alilia kwa maumivu mengi
c) Vielezi vya Namna Kitumizi/Ala
Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani
k.m: kwa kisu, kwa jembe, kwa meno, kwa moto, kwa maji
Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa
d) Vielezi Vikariri
Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo.
k.m: haraka haraka, ovyo ovyo, juu juu
Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo
e) Vielezi vya Ki-Mfanano
Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha.
k.m: kitoto, kiungwana,
Babake huongea kiungwana.
Harida hutembea kijeshi
f) Vielezi Viigizi
Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti
k.m: tuli, chubwi, tifu, chururu
Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi
g) Vielezi vya Vielezi
Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo
k.m: sana, kabisa, hasa, mno
Mamake Kajino alitembea polepole sana.
Chungu kilivunjika vibaya kabisa
h) Vielezi vya Vivumishi
Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi
k.m: sana, kabisa, hasa, mno
Yeye ni mrefu sana
Mtoto wake ana tabia nzuri mno