8:00 PM,Alhamisi 2010
Liwalo na liwe kazembe alikuwa ameamua kumpangia aliyekuwa bosi wake njama.
”Hakuna vile atanipiga kalamu bila kunilipa.”Alinuiza.
Jane alikuwa chumbani mwake akijifisha marashi na kuvaa mini tayari kwenda klabuni kujivinjari.Ilikuwa desturi yake kuponda raha kila Alhamisi kama njia ya kuikaribisha wikendi.Laiti angalijua Kazembe ana nia gani naye usiku wa leo.Dereva wake alimfikisha kwenye klabu ya Peponi na kulitia gari moto tayari kuenda katika hamsini zake.
“Saa sita uje unichukue,”Jane alimwambia na kuondoka kwa mwendo wa batobato.Mini yake ilikuwa imemchukua kama mwanamitindo na kuwaacha wanaume wakiugua homa ya mapenzi kila alipopita.Hungesema ana umri wa miaka arubaini na nne kutokana na urembo na mtindo wa mavazi yake.Waliosema pesa ni sabuni basi hawakukosea.
Kazembe alikuwa ametulia kule klabuni huku akirusha macho yake kila mahali kama kachero.” Aliwaza kisha akainuka tayari kuondoka.'Lazima niende mpaka kwake.'alisema moyoni na kuchukua misamba mirefu kwa hasira.Kinyume na matarajio yake alimsukuma mwanamke mmoja kwenye vidato na kumuwahi mapema kabla hajaanguka.
“Samahani sana,”Kazembe alikuli.
“Tumia macho mburukenge wewe,”Jane alitema maneno kwa hasira na kuinua kichwa chake.Hakuamini kumwona kijana barobaro mwenye ulimbwende na mvuto wa hisia.Kazembe alikuwa njorinjori,mwenye ndevu ndefu kama kalasinga na masharafa na kifua kilichotanuka.Mweusi kama kigongo cha mpingo na sauti nzito.
“Niwie radhi,sikunuia kukuangusha.Nilikuwa nimezama mawazoni.”
“Mawazo ya nini mwenzangu?”Jane aliuliza kwa upole.Kupatana na mvuli kama huyo wa umri wa makamo aliona ni kama bahati nasibu kwake.Kwa muda amekuwa akitumia pesa zake kuwashawishi vijana wenye nguvu na umri mdogo kushiriki anasa naye na Kazembe hakuwa tofauti na hao wengine.
“Shida za kinyumbani na kikazi tu.”
“Mbona usije nikununulie kinywaji?Huenda nikakusaidia kutatua shida zako na pengine kukupa kazi.”
Kazembe alimwangalia Jane kwa macho yenye kiu tolatola.Jane hakuweza kumkumbuka Kazembe kwani mara ya mwisho kuonana ulikuwa mwaka wa 2008 na hakuwa na ndevu wala masharafa.
“Unasemaje?”Jane alisaili na kumtoa Kazembe katika bahari ya mawazo.
“Kama si vileo sina shida.”
“Haya,njoo!”
Kazembe daima hukumbuka kioja kilichotokea mwaka wa 2008 Disemba alipopigwa kalamu na kutolipwa.Alikuwa amegombana na kijana mmoja aliyekuwa akimezewa mate na Jane na bila kujua kijana yule alikuwa akivunja damu.
“Kutoka leo sitaki kukuona kazini.Usidhubutu kukanyaga humu la sivyo nitahakikisha umetiwa mbaroni.”
“Lakini mwenyewe amenitania na kuikejeli hali ya aila yangu.”
“Ungejizuia.Usipojua jinsi ya kutuliza hasira yako utaishi kuhasirika.Halafu ukaambiwa na nani ugeuze mahali pa kazi uwanja wa masumbwi?”
“Bosi,naomba msamaha.Hilo halitarudia tena.”
“Ni kweli halitarudia kwa sababu hutakuwa humu tena.”Jane alisema na kutabasamu akiwa amemwangalia Kijana yule kwa macho yake ya kikombe.
“Tafadhali.”
“Nimesema utoke;na kwa taarifa yako,hakuna senti unapewa.”
“Jane.Samahani,bosi lakini bado sijalipwa mshahara wa mwezi uliopita na mwezi huu unakaribia kuisha.Sijalipa nyumba,hakuna chakula …..”
“Hamrere zako nenda ukazipigie mbali.”Jane alisema na kuwaambia walinzi wamtupe nje na wasiwahi kumruhusu atie miguu yake katika kampuni yake ya riba ya SEFU; 'Securing your Future ilikuwa kampuni ya dada yake aliyeaga kutokana na ajali ya barabarani.Kwa kuwa jina lake lilikuwa kwenye leseni ya kampuni hiyo,alichukua usukani rasmi na kuwafuta wafanyakazi waliokuwemo na kuajiri wengine.
Kazembe anakumbuka jinsi maisha yalivyomwendea benibeni baada ya kumwaga unga katika kampuni ya SEFU . Alishindwa kugharamia mahitaji ya mama yake aliyekuwa akiugua .Kodi ya nyumba ikamshinda na kama hilo halikutosha,kulala ubao ikawa kawaida kama ibada.Kazembe alipatwa na msongo wa mawazo kwa kushindwa kukimu mahitaji yake na mama yake.Ajenti wa nyumba walilazimika kuwatupa nje ya nyumbe yao na kunadi fanicha zao na vitu vingine vya nyumba.
Waliokuwa na vichache wakawa hawana kitu asilani.Maisha yaliwafanya omba omba na masikini wa sina sinani.Mavazi yakawa matambara na chakula kikawa makombo ya pipani.Kazembe aliishi kulia kinyemela ili mama yake asione.Siku moja Mercy alimwita Kazembe.
“Mwanangu,usikufe moyo.Mambo yatatengemaa siku moja.Sitaki kuzidi kuwa mzigo kwako kwa kuwa siwezi kujisaidia kwa chochote.”Alitua kidogo na hatimaye akasema,”Nimeamua kuchukua hatua nyingine.Ninakupenda.”
Ghafla,alianza kutetemeka na kutokwa na pofu mdomoni.Kufumba na kufumbua,alikaa kimya na mtima kuacha kupiga.Kazembe alilia mpaka machozi yakaisha,akasinasina na kubakia kuukodolea macho mwili wa mamake asijue achukue hatua gani.Usiku huo alimpiga mamake chuchuli na kuondoka naye hadi mtoni.Akauvuka na kuingia katika makaburi ya Kipepeo.Udongo ulikuwa mwepesi kutokana na mvua ya kidindia iliyokuwa imenyesha kwa siku tano mfululizo.Alitafuta vijiti na kuchimba shimo dogo na kumshusha mamake polepole.Alimpigia dua na kumzika bila kumwekea lawama ya kumwacha duniani peke yake.Alichukua fungu la mchanga kutoka kaburi moja na kumwekea mamake kisha akaeka msalaba aliotengeneza kwa vijiti juu ya kaburi la mamake.
Follow me on Twitter
@WeyeMatuko
YOU ARE READING
KISASI
General Fiction......Alikuwa tayari ameua maajenti waliowatimua na kunadi vitu vyao vya nyumba,akamtafuta kijana yule aliyekejeli aila yake na kufanya afutwe kazi na kumtupa kisimani.Aliyekuwa amesalia ni Jane.... Anasa/Kisasi/Upendo