SURA YA TATU

0 0 0
                                    

Tumaini alipoketi alionekana mwenye mawazo mengi, mwenyeji wake alimsogea pole pole akitumia mkongojo wake, akasimama kando yake nukta kadha hajanza kuzungumza naye, Tumaini hakuwa ametambua uwepo wake.
"Umeamka salama kweli?!" Bi. Tabitha alimuuliza kwa toni ya wasiwasi.
"Ah! Mama, shikamoo," Tumaini alimuamkua akionyesha mshituko.
"Sasa ni saa nne, lakini hujaanza vipindi vyako," mwenyeji wake alimkumbusha jukumu lake.
"Labda leo wapate mapumziko, aah...jana alikuwa!"
"Nani?"
"Bw. Mfarika, 'kaniambia nijiunge na shule yake. Nami kwa sababu nilijua azma yangu ya kuanzisha vipindi nilikataa lakini makataa hayo yalifanya akanionya."
"Jihadhari naye mwanangu, ni insi mui. Amewatenda mengi wanakisiwa hiki."
"Nimekusikia mama. Itanilazimu basi niache vipindi hivyo, huenda vikanizalia karaha. Mimi mwenyewe mtawa humu."
"Nitazungumza na chifu wetu, labda tutapata msaada wake. Umekuwa taa kwa watoto wetu, huna haja ya kufunika mwanga kwa sababu ya upepo uvumao."
              Baada ya maneno yale, Bi. Tabitha alianza kuondoka kisha kando yake Tabby akatokeza na kopo la uji.
"Leo tumechelewa kuanza vipindi vyetu," Tabby alimwambia baada ya kimya cha sekunde kama tano hivi.
"Maamkuzi kwanza kabla ya chochote maana we," Tumaini alimkumbusha.
"Bibi amenda kwa Bw. Mazoea, lazima anaenda kuzungumza naye juu ya Bw. Mfarika."
"Amefanya nini cha kumzungumzia?."
"Si mwema anavyoonekana chini ya kofia yake na miwani."
"Kwa nini?"
"Yeye pekee hujitakia makuu kisiwani humu. Hataki kuona mtu yeyote akipiga hatua kumzidia. Atamtolea matisho ya barua au afanye kila jitihada kubadili taswira yake katika jamii."
Tumaini alimsikiliza Tabby kwa makini, japo alikuwa mdogo wa umri, alijua mengi kumzidia.
"Alifanya mwanabiashara mmoja aliyekuwa amepanga kuwekeza katika kisiwa hiki akatoweka asionekane tena. Yupo mwanabiashara alinunua shamba ufuoni, akaanza ujenzi mara moja. Lakini kila kukicha vifaa vyake vya ujenzi na raslimali zilikuwa zikipotea, na nyakati zizo hizo ndizo ambazo alijenga shule lake, watu wakasema mali ya yule mwekezaji ndiyo aliyotumia."
"Basi kwa nini watu wasiungane wakamtimua!"
"Ana wale wanaomuunga mkono kwa lolote," Tabby alimjuza, "kuna wazee wanne ambao wanao aliwapeleka mjini kutafuta riziki, hawaruhusu baya kusemwa kwake."
"Wanakisiwa wote wameamua kutawaliwa na vichwa vitano."
"Bw. Mazoea alitishiwa siku moja kwamba huenda akapoteza bintiye alipoanza kufuatilia habari za yule mwanabiashara niliyekufahamisha."

Baada ya maneno yale, kila mmoja alikuwa kimya, Tabby alipiga mafunda ya uji huku Tumaini akiwazia aliyosimuliwa.
                                                ***
            Tumaini alipokuwa amelala, usingizi ulimpiga chenga akasalia kugaagaa kama mtu aliyeumwa. Mbalamwezi ilipenyeza mwanga mpaka alipokuwa. Tabby aliyekuwa kando yake alikuwa amelala fo fo fo, alikumbuka jinsi mjo wa Shata katika kijiji chao ulibadili maisha yake kwa kiwango kikubwa.
Siku moja aliandamana na Mziwanda kuelekea kwa kina Shata kucheza. Shata alipowaona, alienda akamvuta Mziwanda naye akasalia amesimama kama mlingoti. Mziwanda na Shata walianza kucheza kwa furaha.
"Njoo tucheze," Mziwanda alimuita baada ya kumwangalia na kuona alivyokuwa ametokwa na machozi.
"Aka! Shata atanifukuza," alikataa mwito wa mwenzake.
Mziwanda alichukua kigari kimoja walichokuwa wanachezea akampelekea. Shata alipoona vile, aliinuka akaenda na kumsukuma akanguka jiweni.
"Simtaki kwetu," Shata alimwambia Mziwanda, "sitaki kucheza naye."
"Lakini ni mwenzetu," Mziwanda alimtetea akimuinua, "muache acheze nasi."
"Ondoka," Shata alimwambia akinyakua kigari alichokuwa amepewa na Mziwanda, "we' ndiye tuendelee kucheza."
Alianza kulia akamlalia Mziwanda begani.

Shata alimvuta Mziwanda kumuondoa lakini mwenzake akakata kumfuata.
"Humfanyii vizuri," Mziwanda alimwambia Shata akijitoa mikononi mwake.
"Basi nawe kama hutaki kucheza nami ondoka kwetu."
Mara moja Mziwanda alimshika mkono wakaanza kuondoka. Shata alisimama akiwaangalia na vidude vyake mkononi.
"Basi shika," Shata alimwambia Tumaini akimnyoshea kigari.
"Nenda 'kachukue," Mziwanda alimshauri.
"Atachukua tena," alikataa wakiendelea na mwendo.
Maisha yaliendelea kuwa hivyo mpaka walipofika madarasa ya juu. Mziwanda alipokuwa katika darasa la nane, Shata alikuwa darasa la saba, naye akawa darasa la sita.
"Sifurahi kumuona karibu yako," alimwambia Mziwanda siku moja walipokuwa wanaelekea shuleni.
"Hakuna ubaya wowote akiwa nami," Mziwanda alimwambia katikati ya kicheko, "siwezi kumtimua, sote tunatoka mahali pamoja."
"I always feel insecure," Tumaini alimwambia akisonya kwa utani, "always feeling nitakupoteza kwake, kwa sababu hiyo sitaki uwe ukitangamana naye kila mara. Kumbuka tulikoanzia tukiwa wadogo."
"Nime...," kumbukizi zilikatizwa kwa sauti iliyotokea kando yake.

KIZAZI DHALIMU Where stories live. Discover now