SURA YA NNE

1 0 0
                                    

"Kweli kumpenda asiyekupenda ni kama kutikisa umande utiririke kutoka juu ya mti," Shata alimwambia Rehema akiegeza gari lake kando ya benki.
Pasipo na kusema lolote, Rehema alishuka akamuongoza mpaka afisini alipokusudia kuwa naye kwa maongezi.
"Kwa nini usimuache mume wa mwenzako," Rehema aligonga ndipo akijua anatia msumari moto kwenye kidonda, "mshale ambao hujaingia sana si mgumu kuchomoa. Kubali kwamba yalishatokea akampata aliyeumbiwa na Maulana."
Shata alipokuwa ameketi akimsikiliza alimwangalia kwa kijicho.
"Ushapenda kweli kutoka kuzaliwa kwako! Unajua kupenda kweli, 'mi Mziwanda nikampenda ningali mchanga tulipofika kijijini kwao. Nikamfanyia kila alichotaka tukiwa shuleni Tusonge Mbele."
Rehema alimwangalia kwa huruma, alimuona mtu aliyejaza choyo moyoni asimtakie mwingine zuri lolote kumtendekea.
" Wakati huo wote Tumaini alijifunga kwake. Tulipotoka shule ya msingi tukajiunga na shule ya upili ya Hodari, nilifikiri atanipenda mimi lakini kumbe niliudanganya moyo wangu. Nilimdanganya baba kwa ajili yake, nikamlipia ziara za shuleni."
"Umechukulia vipi ziara ya Bw. Brownson katika kampani lenu?" Rehema alimuuliza kubadili mada ya maongezi.
"Baba atafuata aliyoambiwa, hata labda mabadiliko yataanza kuonekana juma lijalo."
"Mimi kwa upande wangu sayansi na teknolojia kuchukua asilimia kubwa katika kazi zetu sipendi, hata kinaweza kukasababisha hasara."
"Usiwe mtu wa kizamani," Shata alimwambia akicheza.
"Ni kweli, ila uzamani na usasa sio hoja, naona heri kusalia katika zama zetu ikiwa usasa kudorora kwa maadili katika jamii yetu."
Rehema alifikia pochi lake akatoa simu kisha akafungua ukumbi wa kulikoni na kumuonesha mwenzake picha fulani.
"Nafikiri haya yatauteka ulimwengu," alimwambia akimuonesha picha ya watalii waluokuwa ufuoni mwa bahari.
Picha ile walipigwa wakiwa na nguo za ndani pekee, kando yao palikuwa na wavulana wa kiafrika wenye umri kama miaka kumi na miwili waliokuwa wakiwangalia, kando yao upande wa kushoto palikuwa na wanaume wazungu waliokuwa wanapeana busu. Kutoka kwa muonekano wao walikuwa walawiti.
"Haya ndiyo unayoita kupiga hatua kimaendeleo," Rehema alimwambia akirudisha simu yake kwenye pochi, "they're eroding our culture."
"Hayo yanakuhusu nini! Wao wamefika kustarehe. Hayo mengine usiyaangalie, wanainua uchumi."
"Wanatupotosha na usasa wao, ndiyo maana hata mwenyewe sipendi mitandao ya kijamii, ni ukumbi wa kulikoni nao ni kwa sababu ya kazi. Mitandao hii inaeneza maovu mengi katika ulimwengu wa sasa."
"Wewe ni mtu mzima, si kwamba wewe ni mtoto asiyejua mbivu na mbichi. Mwenyewe chagua mkondo wa maisha yako."
"Ndiyo mimi ni mtu mzima, ila kwa sasa hata watoto wa umri mdogo wanamiliki simu tamba ambazo zina mitandao hii nao wataiga kila waonacho mtandaoni kiwe kizuri au ki..."
           Mlangoni palibishwa Rehema akaitikia kisha askari wawili wakaingia na kusimama nyuma ya rafikiye.
" She's the one," Rehema alibadilika mara moja, "ndiye aliyempa hundi feki, mchukueni kisha m'mwachilie kijana wa wenyewe."
"Rehema...nimefanya nini..."
"Ulimpa Mziwanda...," Rehema alikataa maneno yake alipoona askari wanampa mgongo na kuanza kuondoka, "mnafanya nini?! Huyu ndiye mhalifu, mchukueni."
"Aliyeleta ndiye mwenye hatia."
Baada ya maneno yale, askari walifungua mlango wakatoka.
"Rehema...unaweza ukaniitia askari?!" Shata alimuuliza kwa mshangao.
"Wewe ndiye unafaa kukamatwa," Rehema alimwambia kwa ukakamavu, "ulilofanya si zuri."
"Hiki kiafisi kisifanye uvimbe kichwa," Shata alimwambia kwa hasira kisha akaondoka.
"Kila mbwa ni simba kwenye himaya yake," alijisemea akifikia tarakilishi iliyokuwa mbele yake, "kweli kuwa na marafiki wabaya kunaweza kukakuzuia kuwa na marafiki wema."
                                            ***
           Asubuhi mwendo wa saa mbili, Ali alikuwa ameshasimama nje ya nyumba ya Rehema akimsubiri waondoke kwa pamoja.
"Kuamdamana na mwanamke katika safari kunataka uwe na subira," alijisemea akielekea mlangoni.
Walikuwa wameagana kuondoka saa moja kwenda mpaka kituo cha polisi kumwangalia mwenzao aliyekamatwa siku iliyotangulia.
"Nakuona bado u mzembe kama nyakati zako za chuoni," alianza kumzomea akiingia ndani ya nyumba.
Kwa haraka, Rehema alitua pochi lake lililokuwa kitandani akatoka nje.
"Mwanangu kuwa na subira, haraka zako siku moja zitakufikisha pabaya," Rehema alimfikia na kumuamkua kwa tabasamu.
"Subira! Mambo mengine hayahitaji subira."
"Subira ndiye mama wa makuu yote," Rehema alimwambia akielekea kwa pikipiki.
Ali alisimama mlangoni akamwangalia alivyokuwa anaondoka akaridhia moyoni.
"Kweli mimi ni shujaa kwa kuchagua," alijisemea kwa sauti ya chini.
"What have you just said?!" Rehema alimuuliza baada ya maneno yale kumfikia kwa mbali.
"Hilo si neno," aliepuka swali la mwenzake.
             Walipanda pikipiki wakaondoka;
"Kweli leo umerembeka," Ali alianza uchochezi juu ya mwenzake.
"Acha za kwako," Rehema alimwambia katikati ya kicheko, "na siku nyingine je?!"
"Huwa umerembeka ila leo imezidi siku nyingine zote. Nilikuonya tukiwa chuo sitaruhusu urudi nyumbani kwa wazazi wako, singeruhusu wewe kunipotea baada ya kupatana kwetu."
Rehema alitabasamu baada ya kusikia maneno yake, tabasamu lenyewe lilikuwa la mapenzi ambayo yaliyokuwa yamekita mizizi kutoka moyoni ikaenea mpaka kwa ubongo wake.
"Utasimama dakika chache nifike dukani kumchukulia maziwa kwa mkate," Rehema alimwambia akionesha duka moja kwa kidole baada ya kufika katikati ya jiji lao.
"Ila kwa leo sitaruhusu uwe karibu yake kabisa. Kutangamana kwako naye wakati mwingine hunitia ngoa."
            Rehema aliondoka akavuka barabara mpaka upande mwingine. Ali aliposalia baada ya mwenzake kuondoka, alianza kufikiri atakalomwambia Mziwanda iwapo atamuuliza kuhusu habari za Tumaini.
"Lakini mwalimu hajamfanya lolote baya...sijui anaitwa Tumaini, yes, ndiyo. Mfarika hafai kumtenda baya," sauti ilimfikia alipokuwa amesimama.
Kwa haraka alisonga karibu na lori lile lililokuwa linapakiwa mizigo apate umbea. Alisonga akaketi kwenye fomu iliyokuwa karibu yao.
"Kwa taarifa yako, mwalimu anawasaidia watoto wetu, vipindi alivyoanzisha ufuoni vimesaidia. Mwanangu kwa sasa anajua kuhesabu, kusoma na kuandika maneno madogo madogo."
"Ni heri arudi alikotoka, sisi huenda tukapoteza kazi. Mimi nionavyo tupo salama kabisa kisiwani hata bila elimu," mwenzake alimpinga, "bora tumepata mahitaji ya msingi kama chakula na mavazi, elimu ni ya baadae."
"Usiwe na mawazo ya kale bwana we, dunia inabadilika, bila elimu hutaweza kufanya chochote. Yeye si kama Bw. Mfarika anayefanya kupata elimu kuwa ghali, yeye anafunza bila karo. Acha kuwa mtumwa na mateka wa bwana wako usione hata mabaya yake. Akirudi jijini humu huenda waliotaka aangamie watamuumiza. Mimi naona heri akisalia huko huko kisiwani." Kwa maneno yale, waliokuwa wakiongea walikabana koo wakatenganishwa na wenzao waliokuwa wakiwasikiza kutoka kazi ilipoanza.
                                                     ***
           Ali na Rehema walipofika karibu na lango la kituo cha polisi, walimuona Shata akiondoka kwa gari lake.
"Akafika kufanya nini maeneo haya?!" Rehema alimuuliza mwenzake.
"Mimi sina uhakika, labda wewe unafahamu kwa sababu ni rafiki yako."
Pasipo na neno jingine wote waliandamana mpaka kwenye masjala wakaandikisha walichotaka kisha wakaondoka na kuelekea ambapo wangepatana na Mziwanda. Baada ya kusubiri kwa dakika tano hivi, walimuona akiwajia, ilivyokuwa kawaida yake alivaa tabasamu usoni.
"Karibuni," aliwakaribisha kwa furaha, nimefurahi kuonana nanyi, asanteni kwa mapenzi yenu juu yangu."
"Tumemuona Shata akiondoka. Alifika hapa kufanya nini ikiwa ndiye chanzo cha haya...," Rehema alimuuliza akionekana mwenye kuchukizwa na kuja kwa Shata.
"Amefika akanieleza kwamba ndiye anayeweza kunitoa humu bila kufikishwa mahakamani. Mwana wa wenyewe 'kanigandia kama gundi. Nimemuonya zaidi ya mara moja."
"Usitie shaka, nimewajuza wazazi wako."
             Walikaa kimya kwa sekunde kadha Rehema akitoa vyakula walivyombebea mkobani.
"Asubuhi tulipokuwa safarini, nilisikia maongezi kutoka kwa watu fulani, sijui kama yanamhusu mkeo!" Ali alivunja kimya, "nilisikia vijana fulani waliokuwa wanapakia gari wakizungumzia mwalimu Tumaini kisiwani Mawe."
Maneno yale yalimfanya Mziwanda kuwa makini hata zaidi.
"Walikuwa wakizungumzia yapi?" Mziwanda alimuuliza alitaka kusikia mengi.
"Walisema ameanzisha vipindi vya kufunza wana wa kile kisiwa, lakini pametokea pingamizi kutoka kwa bwenyenye mmoja kwa jina la Mfarika, na kuendelea na vipindi hivyo huenda akahatarisha maisha yake. Sasa mi' nakushauri ukubali maneno ya Shata ukitoka upate upenyu wa kufika kisiwani mambo yatakuwa salama."
"Kweli we' msiri kwa mwenzio," Rehema alimwambia, "haya yote hukupata kunijuza safari nzima."
"Si kila neno la mumeo unapaswa kujua mke wangu."
             Waliketi pale wakizungumza kwa dakika chache kabla Mziwanda hajaondolewa na askari kurudishwa ndani ya chumb a kidogo kilichokuwa kama makazi yake kwa siku alizokuwa pale.
Chakula alicholetewa na wenzake kilitupwa kwa taka kwa kisingizio kwamba huenda kikawa na sumu au dawa za kulevya.
'Kama alipatikana akiwa majeruhi kisiwani, basi bila shaka ni mke wangu. Naye Shata alitaka kumuangamiza kufaidi nini?! Mtu asiyeweza kuwa mke wa mtu, tabia chanya. Anabugia vileo na dawa kama dunia inamtema leo, mtoto hana adabu kwa mzazi wake, hayo yote anasema uhuru, uhuru usiokuwa na mipaka si uhuru tena bali ni utumwa,' Mziwanda aliwaza Baada ya kurudishwa korokoroni na kuondokewa na rafiki zake.
                                            ***
          Tumaini alipumzika jiweni akifurahia uzuri wa manthari yale, mawimbi hafifu yalikuwa yakitoka ziwani mpaka alipoketi yakaacha vidagaa mchangani viking'ang'ana kurudi majini kuokoa maisha.
Aliangalia katikati ya jua, mwanga ukamzidia. Alikuwa pale kiwiliwili ila kifkra alikuwa akimuwaza mamake, Bi. Linda. Alimhurumia hata kushinda nafsi yake mwenyewe. Alimjua kutoka utotini mwake, alimuona mtu dhaifu kwa kuwajali watu wengine, alikuwa mtu mwenye huruma mpaka wakati mwingine angejiingiza kwa lindi ya shida kwa kuwasaidia waliokuwa karibu yake.
              Alikumbuka jinsi baada ya kukamilisha mtihani wake wa darasa la nane, mwito katika shule ya upili ya Hodari ulimtia mamake mashaka.
'Hatma yetu ni kuwa pamoja,' aliwaza siku hiyo aliyopokea barua kutoka kwa mwalimu mkuu, 'nyavu ya maisha imetunasa tusitengane hata!'
Alikuwa mwenye furaha akijua kwa mara nyingine atakuwa karibu na Mziwanda, alipopiga darubini na kukumbuka kwamba atakuwa na Shata shule moja, furaha yake ilifunikwa na wingu jepesi la huzuni.
"Siku zote mwanga huzidia giza nguvu," alijisemea akitikisa kichwa kujisahaulisha kuhusu hasidi yake.
Nia yake ilikuwa kumuona tena Mziwanda na kufaidi kutoka kwa usalama aliohisi kila alipokuwa karibu yake.
Alipofika nyumbani kwao yalikuwa masaa ya jioni akamkuta mamake akioka moto nje ya nyumba yao ya msonge. Mamake alipomuona alisitisha shughuli yake akainuka kumlaki.
"Umefanikiwa mwanangu?!" mamake alimuuliza akiinuka.
"Ndiyo mama," Alimwangalia mamake kwa furaha, akamkabidhi barua bila kuulizwa.
"Nambie tu mwanangu shule ipi," mamake alimwambia akimrejeshea bahasha.
"Naenda kujiunga na shule ya upili ya Hodari."
"Hongera mwanangu. Mamako nakupa pongezi na shukrani za dhati kwa bidii uliyotia masomoni."
"Asante mama."
"Huko ndiko aliko Mziwanda...mwana wa Bi. Zena?!"
"Ndiyo mama."
"Atakulaki kwa furaha mwanangu, atafurahia kumuona mtu kutoka katika kijiji chao," mamake alimwambia kwa furaha.
             Mamake aliinama akainjika sufuria mekoni, naye akaingia ndani ya nyumba kuweka barua yake.
"Tumaini!" mamake alimuita baada ya sekunde kadha.
"Bee!"
"Njoo mwanangu," mamake aliita akielekea mlangoni, "bintiye Bw. Makali naye yuko kuko huko..."
"Ndiyo mama."
"Basi mwanangu ni heri ubadili shule, kwa sababu ninyi kutoka alipofika kijijini humu hampikiki chungu kimoja."
"Mama, ondoa mashaka. Kwa sasa sisi ni watu wazima, hayo yalikuwa mawazo ya kitoto."
"Hapana mwanangu. Usikanyage usiku miba uliyoona mchana, utakuwa mjinga wa mwisho."
Alipuuza ushauri wa mamake, alikuwa tayari kudungwa na miba kwa sababu ya kufikia ua alilotaka. Jioni hiyo walikula chajio kwa furaha wakizungumzia mipango yake ya kujiunga na shule ya upili ambayo ilikuwa majuma mawili tu mbele yake.






                      

KIZAZI DHALIMU Where stories live. Discover now