Ilikuwa ghafla tu, Pepo kali zilipovuma karibu kila kona ya wilaya ya Kibondo, mkoani kigoma.
Taratibu mawingu mazito yakalifunika anga kiasi
cha kuifanya saa tisa ile ya alasiri ifanane na
usiku wa manane, usiku wa kiza, usiku wa hofu.
Ingawaje ilikuwa ni msimu wa kiangazi na kwamba ni aghalabu mvua kunyesha, lakini
hakuna aliyeipuuza dalili ya mvua ile ambayo ni
mawingu.
Kilichowafanya wakaazi waogope zaidi ni jinsi giza
lilivyozidi kuumeza mwanga, maana hata kama
nd’o dalili yenyewe ya mvua, hii sasa ilizidi!
Baadhi ya wafanyabiashara wakaanza kufunga
maduka yao, wanafunzi wakikimbilia makwao, na
hata mifugo nayo ikaanza kurejea mabandani
ikijua kuwa usiku umewadia. Wale wenzangu na
mimi wenye nyumba za udongo zilizosheheni
‘mawakili’ karibu katika kila ukuta walianza
‘kudhikiri’ vyumbani mwao wakimuomba mola
awasitiri…maana bila hata ya mvua tu, kila siku
ukuta unakuuliza ‘Nikuuwe?’ sasa je ikishuka si
kuta zitageuka biskuti?
Upepo mkali uliendelea kuvuma mithili ya kimbingunga huku baridi kali ikiwa imeshtadi
kwelikweli, cha jabu hapakuwa na mingurumo,
radi, wala manyunyu…ni upepo, Baridi na giza tu.
***
Wakati hali hiyo ya hewa ikizidi kuchafuka, katika
wilaya hiyohiyo ya Kibondo nyumba ya Bi
Masonganya binti Kalukalange ilifurika umati
mkubwa wa wana-ukoo kutoka sehemu
mbalimbali. Watoto, wajukuu, vitukuu na
vilembwe wakiwa wamekusanyika kwa
kukizunguka kitanda cha chuma alipolala Bi
Masonganya.
Ni wana-ukoo hao pekee ndiyo waliokuwa
wakijua siri ya hali ya hewa kubadilika ghafla
katika eneo lote la kibondo. Ni kwamba bibi na
mama yao kipenzi, Bi Masonganya alikuwa
akikaribia kukata roho baada ya kuishi kwa
takribani miaka miamoja na sitini! Kwa kawaida
kifo huja ghafla tu na hakuna anayeweza kupata
taarifa kabla…ila kwa wana-ukoo hawa
walikitumainia kifo cha mama na bibi yao yule.
“Yreeeeeeeew! Watemi woseeee! mizimu yoose!
Makulwa na madoto, na makashindyeee!
Mumsaidie mtu wenu.” Maneno hayo yalitamkwa
kwa sauti kali na babu mmoja aliyekuwa
amesimama pamoja na wana-ukoo wale kisha
akatoa chafya kwa nguvu na sauti kali sana!
YOU ARE READING
TANZIA
Ficção GeralKARIBU KATIKA KITABU HIKI USOME SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUSIKITISHA.....................