Sura Ya Saba

6 0 0
                                    

Kama mgomba  mwanadamu sharti kunyauka na kuipiga dunia teke.

Mzee Moja baada ya kuugua kwa muda, ganga ganga za waganga wa ndani na  nje ya nchi,walimpiga dafrau kuwa aliugua saratani ya kibofu.

Nguvu zilimtariki na misuli kumnyaukia.

Maskini akawa la kuguguna haliwezi sembuse la kutafuna?

Akabaki kulazwa hospitalini kwa majuma yaliyogeuka miezi,na hatimaye miezi kuzaa mwaka mmoja.

Baada ya mwaka mmoja,hali yake iliimarika na akaruhusiwa kwenda kuhudumiwa nyumbani mwake.

Aliambatana na muuguzi aliyenatana naye kama smaku.

Ubavuni mwake daima alikuwa,tayari kumfanyia lile na hili madamu kupunguza mateso yake hata ingawa kwa asilimia nukta moja.

Wakati huu wote Msomi na bwanake walikita kambi pale nyumbani ili kuhakikisha Mzee hakupata upweke wala kuhangaika kwa vyovyote.

Kwa kuwa mauti ni hakika aliyojaliwa mja kutoka kwa maulana,matibabu,huduma bora na mapenzi ya familia hayakutosha kumwondelea kudura.

Maskini kama mgomba ulioambukizwa kuvu, akaanza kuozeana ndani kwa ndani na hatimaye kunyauka.

Chombo chake duniani kikafika ukingoni na kuzamia kuzimu kisionekane tena duniani.

Majonzi si majonzi yalitanda kote.

Simanzi iliyokatika kwa upanga iliwagubika Rebeca na wanawe, wakawa hawambiliki wala kusemezeka.

Mti mkuu ulikuwa umegwa na kama wana wa nyuni,waliyumba kwa majonzi.

Risala za rambirambi zilinyesha kama mvua ya rasharasha.

Si wa mbali,si wa karibu,si wafanyibiashara,si viongozi,si mitandaoni,si katika vyombo vya habari.

Kila aliyemjua kwa njia ya moja kwa moja au kupitia biashara zake,alitumia njia iliyomfaa kumwombelezea.

Siku ya kuzikwa Mzee, shughuli zote ziliganda mjini kwao.

Barabara zote ziliongozana kwenda kwake.

Marafiki na maadui  walifika kwa malengo tofauti.

Maadui kuhakikisha kifo chake na marafiki kumuaga kwa mkono wa buriani.

Umati ulijazana pasiwe hata na nafasi ya kukanyagia.

Kila ulipokanyaga ulikanyaga vidole au kisigino cha mwenza.

Kuheshimu matakwa ya mwendazake Mzee,hapakupikwa mlo,ila maji ya kunyooshea koo tu!

Baada ya hotuba na ibada ya mazishi,wote waliombwa kuondoka, kukabakia watu wa familia na wendani wa karibu.

Mzee alizikwa katika kaburi kiingilioni mwa mji wake.

Kinyago cha Mzee kilicho tabasamu,mkongojo mkono wa kulia,mkono wa kushoto mfukoni mwa kabuti ndefu,kilisimama wima kama bawabu nyuma ya kaburi kulichunga.

Maandishi yaliyomeremeta na yaliyosomeka kutoka mbali,yalipiga kamsa.

Here lies a successful businessman,husband and father.

He was a mentor to many.

From dust we came and to the dust we shall end.

RIP Mzee Moja.

***********************************************************************************************

Itaendelea

HIMAYA YA MZEE MOJAWhere stories live. Discover now