IMMA

1 0 0
                                    

MSIMULIZI: ALEX

"Atakuwa tu, kazimia yahee,... hajitambui tena huyu. Tumuache hapa hatofurukuta, ataliwa na fisi... Afu pingu zitoeni mfunge na kamba" niliweza kuishikia sauti ya kizanzibari ikitoa oda.

"Sawa mkuu! Kwanza fisi wale kulee... wananyemelea tuondoke tu, huyu hawezi pata bahati kama yule sijui ndio S..tivi, sijui nani yule.."
Aliyekuwa amenishika, alijibu huku wananitoa kwenye gunia na kunifungua pingu kisha wakanifunga kamba.

"Hivi huyu ndio alifanya nini!?" Mwingine akauliza.
"Hata sijui, mkuu kasema tu tuhakikishe kafa kabisa, na asipatikane milele hata DNA, itakuwa na yeye katoboa siri zao huko... Watajijua wenyewe" yule jamaa mwenye lafudhi ya kiarusha alisema.

Tangia wananiteka huyu jamaa aikuwa anahakikisha siteseki. Aliwazuia wenzake kunipiga akiwaambia nitakufa tu kwani kwenye hii mbuga wanayonipeleka sio rahisi kutoka. Siwezi sana kumsifia, kwani ni muuaji tu kama hao wenzake ila sio mtesaji inavyooneka.

Nilisikia wakimuita kwa jina moja tu kama Imma. Pia walikuwa wakipiga story kuwa wameshawaua wengi tu na Imma ndio mtaalamu wa kuua. Ila kuna huyo anayeongea kizenji, yeye anaitwa kama Koplo Salim, anaonekana yeye ni mtu fulani kwenye Jeshi la Polisi na anatumika kwenye haya mambo.

Wakati nasikia wengine wakibamiza milango ya gari, hapa chini bado nipo na huyo Imma. Ananifunga kamba huku anazichukua pingu. Kisha akaninong'oneza.

"Oya... We jamaa, sijakufunga hiyo kamba, nimeiegesha tu,... Ukisikia gari imeondoka, kimbia mbio huko gari ilipoelekea, kuna jamaa atakuwa anakusubiria na boda, maelekezo mengine atakupa" akanilegezea kitambaa kilichonifunga macho, "ukichelewa kidogo tu utaliwa na fisi, sawa Alex?"

Nilitikisa kichwa kukubali, moyo wangu bado hujatulia. Sina nguvu za kukimbia hiyo kasi ila naamini nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu. Sipo tayari kufia huku mbugani.

Niliposikia tu gari limewaka, nilijifungua kamba haraka na kutoa kile kitambaa kichwani. Kweli panatisha sana hapa porini. Ni usiku wa giza totoro. Sauti za fisi na wadudu ndio zinasikika tu. Kichwa kinaniuma sana, njaa nayo imenimaliza nguvu.

Sasa niliamka nikajijaza nguvu, nikaanza kukimbia kufuata ule mlio wa gari, japo sioni vizuri lakini nashukuru Mungu, nilikuwa nafuata njia. Niliongeza kasi kila napohisi kuna kitu kinanifuata, sijui nguvu zilitokea wapi, kila mlio wa gari unapofifia nilijikuta nakazana na kupata nguvu za kukimbia kwa kasi.

Sasa nikafika mahali ambapo naona barabara ya lami kwa mbali. Nilijua ni lami baada ya kuona magari yakikatiza japo kwa uchache.
"Alex...!!!" Nilisikia sauti ikiniita kwa nyuma yangu, nilishtuka kidogo kujikojolea. Niligeuka nikiweka mikono juu, kujisalimisha.

"Hey! Usijali mi sio mtu mbaya. Imma kanielekeza nikuchukue.." yule braza aliniambia, nikajua sasa nipo sallama japo sina uhakika kama kuna huo usalama. Sijali tena chochote, kwani nimeshakiona kifo tangia natekwa, nishasali hadi sala zangu za mwisho. Kwahiyo nasubiri tu wakati wa kufa unifikie.

Nilimfuata huyu jamaa, nikapanda pikipiki yake, haikuwa hizi za kawaida, ilikuwa ni zile za masafa marefu, kwa hiyo huyu sio bado boda kama nilivyofikiria mwanzo.

Mwendo wa kama masaa manne hivi. Kulikuwa kumeshaanza kupambazuka. Jamaa akaingia kwenye njia moja ambayo ni kama inaachana na makazi ya watu. Tulifika hadi kwenye mto fulani na tukasimama.
"Shuka, tumefika!" Aliniamuru, nilishuka na kukimbilia haraka kwenye ule mto, nikanywa maji kama kichaa. Sikujali ni masafi au machafu.

Dakika tano hazikuisha, gari aina ya Range Rover ilipaki pale nilipokuwa na huyu jamaa wa pikipiki. Alishuka kijana mmoja mtanashati sana, ameshikilia bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti.
"Oya vipi Alex" sauti yake sio mpya maskioni kwangu, ni yule Imma.
"Safi asee mkuu!" Niliitikia kwa sauti ya unyenyekevu.

Gafla alimnyooshea bastola yule jamaa wa pikipiki, nikajua ni utani. Lakini kufumba na kufumbua alimpiga risasi ya kichwa na kumpiga risasi nyingi za kila mahali. Nilipiga magoti nikanyoosha mkono kusalimu amri ambayo sijamrishwa bado. Nikajua huu ndio mwisho wangu.

Hakuniongelesha akaifuata ile pikipiki kisha akaitia moto, ikiwa inawaka akaniita, nikamfuta.
"Shika miguu tumtupie huko mtoni!"
Nikiwa natetemeka sina hata nguvu, nilishika miguu ya yule jamaa na yeye akashika mikono tukamtupia kwenye ule mto. Mwili wake ukasombwa na maji ukapotea.

Pikipiki ikateketea kabisa na mabaki tukayatupia mtoni.
"Kwa sasa ni watu wawili tu wanajua kuwa upo hai..." Aliniambia akiwa amenishikilia bega. "Mimi na wewe tu, ndio tunajua kuwa upo hai.."

ITAENDELEA.

THE COMEBACK Where stories live. Discover now