KWAHERI LAAZIZI

3 1 0
                                        

Leo itakapokuwa jana
Na jana kuwa juzi
Juzi itasahaulika
Na mengi tuliyoyafanya pamoja
Ni bayana kuwa tutayasahau

Mwanzo tutakumbukana
Utanikumbuka kwa moyo legevu
Wenye chembechembe za mseto wa hisia
Lakini jinsi ambavyo siku zinapozidi kuyoyoma
Mahaba yako bila shaka sharti yatasalimu amri
Na utanisahau na yote hayo yatapita

Mwenzio uendako sifahamu
Safari yako ya mbali ishang'oa nanga
Nami sina budi ila kukuaga na majonzi moyoni
Kwa kuwa hatima yako mwenzio si kafu yangu

Laazizi mema usio kifani nakutakiya
Maisha mazuri yenye amani na mafanikio
Ndiyo furaha yangu kwako ewe mpenzi
Siku zako zitawaliwe na siha njema laazizi

Naweka wazi shahidi moyo wangu
Umeniwacha na donda
Asilani lisilo na tiba
Ila natumai nami siku moja
Nitampata mwandani wangu
Awe fundi wa raha zangu
Na mpenzi wa roho yangu

Na siku zikiruhusu sisi kukutana
Nitakusalimu na bashasha usoni
Kwa kuwa sina kinyongo nawe mpenzi
Nenda salama laazizi
Jalali akujaliye mazuri uyatafutayo

My Unknown LoverStories to obsess over. Discover now