Malaika: Mjoooooombbbbaaaaaaaa
Latoi: Malaika
Malaika alimrukia mjomba wake kwa nguvu na kumkumbatia, alihisi kama ghafla tu jua limepambazuka wakati wote huo wa wiki mbili kulikuwa na usiku mnene kwenye maisha yake. Kumuona mjomba wake kulileta faraja kubwa ya ajabu ndani ya moyo, isiyotegemewa. Kijiji kizima kilikuwa hakina matazamio kwamba kuna siku Latoi mjomba wake Malaika atarudi tena kijijini hapo.
Mzee Oldei alikuwa anafahamika sana kutokana na nyumbani kwake peke yake kijiji kizima kulikuwa na luninga, alikuwa ni mzee tajiri na aliyefahamiana vyema na wenyekiti wa vijiji na mpaka baadhi ya wafanyakazi katika ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Na hata huyo mzungu aliyeondoka na Latoi alikuwa anakaa kwenye moja ya nyumba za wageni za Mzee Oldei. Mzee Oldei akiwa na siku ya nne baada ya kupokea simu mpya aliyonunuliwa na mtoto wa kwanza kutoka kwa mke wake wa tatu ambaye yuko masomoni mkoani Arusha, ndipo msiba ukatokea. Mzee huyu alifanya bidii kutafuta namba za yule mzungu alizoziacha kwenye nyumba yake hiyo ya wageni na kutuma ujumbe mfupi uliosema SHEMEJI YAKO AMEFARIKI. Kwa bahati nzuri ujumbe huo ulimfikia mzungu huyu anaitwa Lenny na baadaye Lenny akamwambia Latoi kuwa na ujumbe umefikia kwenye simu yake lakini hakuelewa kilichoandikwa humo. Baada ya Latoi kuangalia, aliamua kumpigia simu Mzee Oldei na ndipo alipopata ufafanuzi wa ujumbe ule na kuambiwa kuwa hata dada yake alishafariki dunia. Usiku mzima hakulala alilia sana na kuamua kupanga safari baada ya siku kumi kwenda kijijini kwao, dhumuni likiwa ni kumchukua Malaika maana alijua ndio mtoto pekee dada yake aliyejaaliwa kuwa naye hivyo binti huyu alikuwa kwenye majonzi makubwa sana.
Latoi
Niliondoka kijijini kwetu miaka mitano iliyopita na mdada mmoja wa kizungu aliyetokea kunipenda sana. Mzungu huyu aliitwa Lenny alikuwa anakaa Toronto Canada na alikuwa ni mwana-anthropologist kwenye chuo kimoja cha hapo mjini Toronto. Nilijifunza kingereza na baada ya miezi sita nikawa nakijua, na kisha tukaamua kuoana na Lenny kutokana pia na shindikizo la wazazi wake Lenny ambao nao walikuwa wanakaa Canada lakini mji tofauti. Baada ya miaka miwili Lenny alinitafutia kazi kwenye studio moja ya kupiga picha wakati naendelea na kujiendeleza zaidi kielimu kwasababu niliishia kidato cha nne tu shule ya kata ya Orkesimet na kuambulia sifuri. Baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mzee Oldei na kuambiwa mipango ya ndugu wa shemeji yangu niliharakisha kupanga safari na kuamua kwenda kijijini nikamchukue Malaika. Kabla sijaenda Canada dada aliniambia
"Kwasababu sisi tumezaliwa wawili tu, basi naomba nikifa mimi wewe uwalee watoto wangu, na mimi ukitangulia wewe nitawalea watoto wako".
Malaika alikuwa na miaka mitano wakati naondoka lakini alionyesha upeo mkubwa sana wa akili na alikuwa na heshima kwa watu wote, hata kijiji kilimpenda ilikuwa sio sawa alishie kuwa mke wa kumi na moja wa Mzee Oldei ambaye alikuwa akijitamba sana kuwa wanawake wazuri wote hapo kijijini ni wake na ilikuwa imebakia Malaika peke yake. Nilijivunia sana mtoto wa dada yangu huyu na hivyo sikutamani kabisa ateseke wala kuumia wakati mimi bado niko hai. Nikiwaza haya niliona usiku mrefu mimi kuanza safari baada ya maandalizi yaliyonichukua siku kadhaa maana ilibidi pia niwape taarifa ofisini na kupewa ruhusa ndio nisafiri. Baada ya mambo hayo yote na pirikishani za hapa na pale kule Canada ambako nilikuwa naishi na Lenny nilisafiri na nilifika kijijini, na kuambiwa walihama na kuelekezwa kijiji cha jirani. Maisha ya kuhamahama kwetu ni kawaida kwahiyo sikuwa na wasiwasi, nilifika kijijini hapo mchana wa saa 6 na kuelekezwa nyumba waliyokuwa wanaishi dada yangu na shemeji yangu. Nikijongea taratibu nilikuwa najiuliza hivi naweza kumkumbuka vizuri Malaika, wakati naondoka alikuwa na miaka mitano tu, sasa atakuwa na miaka kumi, atakuwa amekuwa na kubadilika sana, na ukizingatia wanawake wanakua haraka haraka sana. Niliona kabinti kamejiinamia kanaonekana kenye mawazo mengi sana, na ni kama vile hakuniona nilivyokuwa najongea. Sikusita nikaendelea kutembea kuelekea nyumba hiyo ambayo nilielekezwa na wanakijiji kuwa ndipo anapoishi sasa Malaika kwahiyo nilijua kama hatakuwa yeye basi atakuwa anajua alipo Malaika. Nilipozidi kukaribia binti huyu aliinua kichwa, na nilipouona uso wake sikuwa tena na shaka nilijua ni yeye, alisimama na kunikimbilia na kunikumbatia kwa furaha sana. Alikuwa amebadilika amekua lakini alizidi kuwa mrembo, alimpita mama urembo, na alimzidi baba yake kwa kuwa na kope nyingi, vishimo vidogo kwenye mashavu viliupamba vyema uso wake. Siku zote Letoi alikuwa anajivunia kuwa amemrithisha Malaika kuwa na vishimo vidogo mashavuni kwani wazazi wake walikuwa hawana. Wakati yeye akiwa na furaha kama mtu ambaye ameona jiwe la dhahabu, mimi nilisikia maumivu kwenye kifua kama ndio yanaanza upya na taratibu matone ya machozi yalikuwa yananitoka. Niliendelea kumkumbatia Malaika ili asione kama machozi yananitoka kisha nikayafuta na kuanza kuongea naye.
YOU ARE READING
MALAIKA
Short StoryMalaika alikuwa ni msichana mrembo sana aliyepata nafasi ya kutoka kijijini kwao Mbulu kuikimbia ndoa wakati akiwa mtoto na kwenda kuishi na mjomba wake nchini Canada. Maisha yalikuwa ni mazuri mpaka alipoamua kuyaharibu baada ya kukutana na kuwa n...