Matuko alienda matiti mpaka ghorofa ya nne huku akiingia kila nyumba bila hodi.Pumzi zinamwenda mbiombio kama mja aliyekutana kititi na ibilisi.Simanzi ya kumpoteza mpenzi wake imemwingia mishipani nusura aanze kutiririkwa na machozi.Laiti angalijua Maria si msichana mbeja kama alivyomwona.Sitakuwa nikitia chumvi sana kusema kuwa penzi hili ni kana kwamba lilikuwa la kulazimisha,halikuwa penzi la kweli.Sote tunafahamu uchungu wa mapenzi ambao humpiga mtu kwa nguvu na kumvuruga kimawazo.
Mara tu akasukuma mlango uliokuwa umekomelewa kwa nguvu kupita kiasi mpaka ukavunjika.Akaanguka sakafuni pu! Kama gunia shibe la mahindi.Wakawa wanaangaliana ana kwa ana na Kelvin;mmoja wao huzuni imemkaa usoni, mwengine hasira.
"Akili zako timamu?"
"Ndio,zi razini kabisa.Nyie ndio mnataka kumuua mpenzi wangu!Sivyo?"Hasira ilimtoka Matuko na kusafiri jumba lote.
Papo na hapo Kelvin akajua aliyekuwa akirejelewa.Hasira aliyokuwa nayo ikazama na kuanza kuongea kwa upole ungedhani ni padri akitoa nasaha.
"Samahani mwenzangu,naona umekosea mlango manake humu tu wawili tu,mie na mpenzi wangu."
"Mpenzi yupi?aliyening'inia dirishani?"
Kelvin alijua mambo yameharibika na kumwendea segemnege.Akaanza kumsihi Matuko atulie na kuzungumza kwa sauti ya chini kwa kuwa alihofia Monicah atapata taarifa hii.
"Ninege nipite hadi humo chumbani.Lazima nidhibitishe maneno yako."
"Humo huingii hata kwa mtutu wa bunduki.Mpenzi wangu anatikita na kwa taarifa yako yeye hulala kama alivyotoka tumboni mwa mamake."Aliongopea Kelvin.
"Haya basi,tangulia humo umfumbe kwa mashuka ukiweza halafu nifuate nyuma."
Kelvin alipoona kuwa Matuko ana kila jibu na yuazidi kuwa mbishi,akaamua kutumia nguvu.Alimsukuma kwa hasira na kujaribu kumbeba hobelahobela kumtupa nje lakini wapi! Matuko alikuwa kifyefye na mrefu kama mlingoti lakini mwenye nguvu kupita kiasi.
Kivangaito kiliibuka baina yao ikawa ni patashika nguo kuchanika.Kelvin alirusha dondi kwa hasira na kumpata Matuko puani.Akamgalagaza sakafuni na kumlima magumi yasiyokadirika kiasi kwamba damu ikamtoka puani na mdomoni kama maji kwenye mfereji.Mtoto wa watu akalegea na kubaki pale kinyonge asijue kuwa hapa hakuna shufaka hata kidogo.Amelimwa magumi mpaka mwili ukatibwirika.Alionekana kukaribia kukata roho kwani Kelvin alizidi kumpiga kama mbwa aliyetabawali msikitini.
"N..ni..niue."Aligugumiza baada ya kumunyamunya kwa muda.
"Sina haja lakini ikibidi sitafikiria mara mbili."
Kelvin alimshika kwenye ukosi wa shati na kumburura kwa madharau na kumtupa nje.
"Kama wewe ni mwanaume kamili jaribu kurudisha hiyo miguu humu."
Matuko alitaka kumtusi akashindwa.Hana hata nguvu ya kuongea.Alitaka kupiga ukemi lakini angewezaje?Hata angekuwa na uwezo hangepiga manake aliwahi apa kuwa hawezi piga mayowe liwe liwalo.Pengine awe mwendawazimu.
Kelvin aliurudisha mlango baada ya kupangusa damu iliyokuwa imetapakaa sakafuni.Moyoni anajihukumu kwa ukatili na ushaufu alionao.Alitaka kumpa Matuko pole lakini hakutaka uovu wake umebainike.Hakutaka Monicah ajue tabia zake mbi hata kwa bahati mbaya.Fikra za Maria zilimrudi na kuanza kusumbua utulivu wake."Nitafanyaje kumtoa pale dirishani ilhali Monicah yu chumbani?"Alijiuliza.
Aliwaza na kuwazua jinsi atakavyofanya na hatimaye akaamua kumwita Monicah sebuleni wasuluhishe sintofahamu zao.
"Monicah."Aliita kwa nguvu.Dakika tatu hivi zikapita bila kupata sauti yoyote ikiitika.
"Mpenzi njoo tutatue tofauti zetu.Monicaaaaah."Aliita tena huku akijaribu kutia madaha ili kumpumbaza.Hamna jibu.Akaamua kwenda hadi chumbai amkunyue waje sebuleni.
Kitandani majuto na uchungu ulimbwaga Monicah.
Kisu kimechomekwa kitovuni.Damu imeshamiri kwenye mashuka meupe na kubadili rangi na kuwa mekundu.Maskini mtoto wa watu anapepesa kope kwa shida.Bado machozi yanamtoka kwa wingi;si machozi ya uchungu wa kisu tumboni bali ni uchungu wa mapenzi.
Kelvin aliusukuma mlango taratibu.
"Monicaaah,"akaita tena huku anapinda shingo kuangalia ndani.
Ahsante kwa kusoma mpaka hapa.Ningependa kusikia maoni toka kwenu.
Vote and comment♥
YOU ARE READING
Nisamehe Mpenzi
Short StoryMatuko atafanyani agunduapo kuwa Maria ni msaliti? Monicah atafanyani agunduapo kuwa Kelvin ni msaliti?