Nisamehe Mpenzi(viii)

31 0 0
                                    

Maria na Kelvin walikuwa katika vyumba tofauti katika kituo cha polisi.Hakuna aliyejua kitakachojiri baadaye manake imepita siku nne bila kuzungumza na wakuu wa polisi.Waliweza kupewa uji uliopikwa kivoloya wakati wa asubuhi na jioni kula ugali ambao haukuwa tofauti na uji waliopata kunywa asubuhi.

Maisha yalionekana kuwa magumu kwao.Maria aliishi kwa kwikwi tu akijaribu kuwaambia askari jela kuwa yeye hana hatia yoyote.Gereza alilokuwa kulikuwa na wanawake wengine wanne na msichana mmoja apata miaka kumi na minane hivi.Kila mmoja wao alikuwa na kesi iliyostahili uchunguzi wa kina kisha ripoti iandikwe kwa idara ya kupambana na uhalifu ili iwapo hawana hatia waachiliwe.

"Hata ulie damu hakuna wa kukusikiza.Mimi nimekaa humu wiki mbili na bado nangojea uchunguzi ukamilike.Hata mimi sina hatia yoyote bali ni kusingiziwa tu eti nilihusika na mauaji ya mtoto wa mwajiri wangu.Sasa acha kuigiza na utulie kwa kuwa askari waliohuku ni sawia na viziwi."

Maria hakutaka kuongea na yeyote mle gerezani hata baada ya kudukuliwa hali ilivyokuwa mle ndani.Kilichomuudhi zaidi ni kuwa hakuruhusiwa kuingia na viatu vyote mle ndani,hakuwa na sweta na humo ndani hamkuwa na magodoro.Baridi iliwatafuna bukrata wa ashiya bila huruma na kuwaacha wakitetemeka  kama makinda wa nyuni walionyeshewa.

Upande mwingine Kelvin alitulia kama maji mtungini.Anafahamu fika kuwa ataachiliwa huru hata ikimchukua miezi mle ndani.Kamwe haoni  sababu maalum inayoweza mfanya ahukumiwe kifungo.Anachojua ni kuwa yu pale gerezani kusaidia katika uchunguzi wa kisa kile.

"Maria,"sauti ilisikika ikiita huku ikikaribia lango la gereza.Kwa furaha,Maria alinyanyuka aste aste na kuelekea mlangoni alipoona ukifunguliwa kwa fujo.

"Kwani umezunguka mbuyu?Iweje ulifika humu nyuma yetu na kupata abra ya kuhojiwa wa kwanza?"Msichana aliyekuwa ameketi kitako sakafuni alisaili.

"Pesa huvunja milima eti,"Aliongezea mahabusu mwengine kwa magigimo.

"Toka nje!"Aliamuriwa na muda si kiduchu alikuwa ameketi kitini.Mbele yake Inspekta mkuu wa polisi pamoja na wanapolisi waliokuwa wamebobea katika taaluma ya saikolojia;uwepo wao ni kuweza kubaini iwapo Maria atawapiga mlazamlaza atakapokuwa akihojiwa.

Maria aliwaangalia kwa macho ya bezo nusura asonye lakini akakumbuka vichapo ambavyo washukiwa wa uhalifu hupata wakati wa kuhojiwa ili wakubaliane na yote watakayoulizwa.Haijalishi iwapo una makosa au la,cha muhimu uwape muda mwepesi nawe upate kichapo cha huruma!Yote tisa,humu gerezani hakuna haki kwa mafukara wanyonge.

Binti huyu alikuwa ameamua liwe liwalo,lazima atamsingizia Kelvin.Hakuamua kufanya hivi ili awe huru,bali ni hasira aliyokuwa nayo kwa sababu Kelvin alimkana na kumpendelea Monicah.

"Majina kamili,"kimya kilivunjwa na Inspekta.

Nisamehe MpenziWhere stories live. Discover now