KARATA YA MAHABA

16 0 0
                                    

John hakujua kuwa uamuzi wake wa kumpenda Hadasa ulikuwa sawia na kushika mapindi ya nyoka.Wendani wake walijaribu kumwonya dhidi ya kujihusisha na uhusiano wowote na binti huyu lakini wapi.Wosia wao ukaingilia sikio la shemali na kutokea la yamini.Alikuwa ameamua kujaribu kuona iwapo mahaba yao yatachanuka kiasi cha wenzake kumlilia ngoa.

Hadasa alikuwa banati njorinjori mwenye urembo wa tausi,miondoko ya njiwa na sura yenye mvuto wa aina yake.Alipenda kuvaa sketi na kuyaanika mapaja yake ya rangi ya kahawia na kuwaacha wanaume wakivunja shingo.Kifua chake kilipendeza machoni mwa kila mwanamume kiasi kwamba wasichana wengine walimwonea gere.Leo hii alikuwa akijipamba kwenda kukutana na mpenzi wake wa wiki mbili sasa,John.Walikuwa wameamua kukutana katika bustani ya  Anasa kurusha nyoyo zao na kufurahia ujana wakati mifupa ingalipo.

“Leo umechelewa kwenda kazini.Huoni ukipigwa kalamu?”

“Usitie shaka,nilishaomba ruhusa ya kutoenda kazini leo.Isitoshe hakuna kazi nyingi leo manake mwajiri alisema maduhuli aliyoagiza hayajafika.”

“Unajipamba ukienda wapi ?”

“shughuli zangu za faragha tu.”John alimdanganya nyoko yake na kumpa busu shavuni na kuondoka tasihili.
Njiani alikuwa akitunga na kutungua ni vipi ataweza kumpa raha na kumfurahisha Hadasa kwa kukubali kujitosa katika bahari ya mapenzi naye.Hakutaka ajutie kumpenda miongoni mwa wanaume wote waliokuwa wakimmezea mate.Aliingia kwenye mitandao ya kijamii na kutafuta maswali ya kila nui ambayo aliona yataweza kumpiga jeki kuanzisha na kuendeleza mazungumzo yao na kadhalika.

Chini ya dakika kumi alikuwa amefika Katika Bustani ya Anasa na kuchagua mahali palipokuwa na miti na maua ya miwaridi.Chemichemi ya maji kando yake na viti  vya buluu vilivyokuwa kando ya meza ya gilasi.
Kufumba na kufumbua Hadasa alikuwa keshafika na kusimama mbele yake.Leo hii kavaa sketi ya Nyeusi  iliyomfika magotini,Shati  nyeusi iliyokataa kuficha 'machungwa' yake yaliyojaa na kusimama kifuani tisti kama mpunga kondeni na viatu vyeusi.John alimchuja  toka usoni hadi miguuni na kuhisi amehamanika ila leo hii alikuwa jambo alilotaka kumwambia.

“Stunning.”John alikuli na kumpiga busu mdomoni kisha akamvutia kiti aketi.Walikuwa wakitazamana kama malimbukeni bila kusema chochote,kila mmoja akifurahishwa na maumbile ya mwenzake.
John  alikuwa mwenye kimo cha wastani,mweusi kama kizimwili na masharafa yaliyopendeza.Kichwani nywele mtindo wa rasta zimemkaa sawasawa.

Mhudumu mmoja alifika na kuwaomba waagize wanachotaka.

“Nipe sharubati..”

“Mimi pia.”Hadasa akarukia kabla John hajauliza alichotaka.Mhudumu alitabasamu na kuondoka.

“Unaonekana mwenye wasiwasi sana,”Hadasa alivunja kimya.

“Si kitu ni mawazo ya kawaida tu.”

“Mawazo yanayotokana na wenzako kukusambika kukatisha uhusiano wetu,sivyo?”

“Hadasa..”

“Ningependa ukiniita baby au jina jingine lenye mnato wa kimapenzi.”Hadasa aliyalegeza macho na kuishika mikono ya John na kuchezacheza nayo kimahaba.Mhudumu alifika na kuwatilia sharubati katika gilasi na kuondoka.

“Kuna jambo nilitaka kukuambia uso kwa uso badala ya kutumia jumbe za simu.”John akavuta pumzi na kupiga funda la sharubati.

“Jambo gani hilo.”

“Kuhusu ndugu yako,Abdul.”

“Ana nini tena?Nildhani nilimwonya dhidi ya kujishengesha na maisha yangu.Alikuambia ukae mbali nami?”
John aliingia mfukoni na kutoa rununu yake na kumpatia Hadasa asome jumbe alizokuwa ametumiwa na Abdul huku akiendelea kuikunywa sharubati yake taratibu.Hakutaka kuandika wa mate na wino upo.Muda huu wote bado Hadasa hakuwa amepiga funda hata moja.Hadasa alizisoma jumbe zile taratibu na kwa makini.Kadri alivyozidi kuzisoma ndivyo uso wake ulivyozidi kujaa mafuta asielewe mbona ndugu yake awe mkatili kiasi hicho.Alimrejeshea John simu yake na kuangusha uso wake kwa hasira na bila kutarajia,mtoto wa watu akaanza kulia.

“Usilie tafadhali.Nilishakiri kuwa mimi ninakupenda na sitokuacha hata kipi kitokee.”

“Nilidhani ulipanga tukutane ili turushe nyoyo zetu lakini ukaamua kuiharibu mwenyewe ili upate sababu ya kuondoka maishani mwangu.”

“Futa hayo mawazo kwa sababu yanakuchosha tu.Mimi sijasema ninaondoka maishani mwako.Kukuonyesha jumbe hizi ni kumaanisha sitakuficha chochote maishani mwangu.Sidhani ni jambo la busara kukuficha swala kama hili.”
Aliendelea kulia huku akigongagonga meza na kutikisa mguu wake kama mtu aliyekuwa akipanga kitu akilini.Jonh Akasimama na kwenda kukumbatia na kutumia hanchifu yake kumpangusia machozi.Simu ya John ikakiriza.Kuangalia ni nambari ya siri.

“John hapa,naongea na nani.?”

“Naona una kichwa kigumu sana na huoni hata ukionyeshwa kitu.Nilikuambia nini kuhusu uhusiano wako na dadangu?Endelea kucheza karata na maisha yako.Utalia kilio cha mbwa mdomo juu na kujutia ukaidi wako.”

John alisimama upesi na kuangalia katika kila dira ya Bustani ya Anasa kujaribu kuona iwapo angeweza kumtia Abdul machoni.Alikuwa na hisia kuwa lazima yuko karibu na genge lake la wahuni.

“Kuna nini?”Hadasa alisaili.

“Aah,ningependa kuondoka.Kuna jambo la dharura limetokea.”

“Twende pamoja,huenda nikawa mwenye msaada kwako.”

“Pengine ukikaa mbali nami ndiyo msaada aula kwangu,samahani sana.”John aliondoka na kumwacha Hadasa akiwa amepotea mawazoni.Moyoni alihisi mfundo dhidi ya ndugu yake,akilini anahisi kuwa anakonda kwa mawazo kila uchao.
'Utakiona cha mtema kuni,' Hadasa aliwaza na kuondoka bila kulipia sharubati kama alivyofanya John.

KARATA YA MAHABAWhere stories live. Discover now