Imepita takriban wiki tatu tangia John na Hadasa kukutana.Alikuwa amefanya uamuzi wa kujitenga kabisa na Hadasa kwa kila hali.Aliamini kuwa penzi hili kumwepuka lina heri naye kwa kuwa ni wazi kuwa uhusiano wao haukuwa mbali na kukalia kijumba cha shetani.Babake alikuwa ameketi kitako kwenye stuli akifuatilia habari kuhusu kesi ya Katega kortini ambayo ilikuwa ikikaribia tamati kwa kukosekana kwa mashahidi na habari kuwa video ile haipatikani hata kwenye kituo cha runinga ya Leo.
Jaji hakuwa na budi isipokuwa kuifutilia mbali kesi ile na Katega kuwachiliwa huru na kutembea mzofafa kama mja aliyetakasika na dhambi.
“John,njoo.”Matani alimwita mwanawe.
“Kuna nini baba,leo hata sipumziki hata kidogo.Nikiketi kidogo mama ananiita,dakika chache baadaye..”John alikata maneno yake macho yake yalipotua wajihini pa babake.Hajawahi kumwona akiwa katika hali kama ya leo.Pafukapo moshi pana moto.
“Bado unawasiliana na mpenzi wako?Sistahili kuhusika sana na mambo yako ya kibinafsi lakini naona ni vyema kujua.”
“Tulitokana wiki tatu hivi zilizopita.Sintofahamu za hapa na pale kati yangu na ndugu yake zilichangia yote.Sina nyemi naye tena.”
“Yeye mwenyewe anajua au ni fikira zako kuwa mmetokana?”
“Haijalishi iwapo anajua.Kunyamaza kwangu kunastahili kuwa dalili kuwa sina hamu naye tena.”
“Kunyamaza kwako kunampa tamaa ya kutaka kukuona na kukutana nawe.Afadhali umpigie simu au umtumie ujumbe umweke peupe .”
“Lakini baba,mbona inaonekana unapiga jeki kukatisha uhusiano wangu na Hadasa?Wajua hata ndugu yake alinitishia uhai ndiposa nikaachana naye?”
“Jibu mwafaka unalo mwenyewe.”
“mbona usiniambie paruwanja badala ya kusema kwa mafumbo nisiyoelewa?”
“John,hakuna mafumbo hapa.Iwapo Abdul anakutishia maisha ili uwachane na Hadasa,ni sababu gani nyingine mie nisichangie mwachane?Hiyo ni sababu tosha ya kuondoka maishani mwake.Isitoshe,kuna wasichana wengi sana hata wazuri kuliko Hadasa.”
“Kuna jambo ambalo unanificha na nitalijua siku moja.”John aliondoka na kwenda kumsaidia mamake kuanua ngano.
Wakati huohuo Matani akaona runinga moja ikipeperusha habari za rambirambi kwa ndugu,jamaa na marafiki wa aila ya Opondo.
“Habari zilizotufikia ni kuwa mwanahabari shupavu wa upelelezi wa runinga ya Leo alikunywa sumu baada ya kumtia mkewe mjamzito kitanzi kwa kumkatakata kwa panga.Wamemwacha mtoto mdogo wa kiume wa miaka mitano….”Matani aliizima runinga na kuondoka.Akalitia gari lake moto na kufululiza moja kwa moja hadi kwenye baa moja ya rafikiye waliyesoma naye chuo kikuu cha Songa.Aliagiza bia ya Jonywalker na kuikumumia kwa hasira na majuto akijaribu kuondoa uhalisia kuwa yeye ndiye kiini haswa cha kifo cha kakake.
Matani alikunywa hadi akakopa bia nyingine nyingi akiahidi kulipa baadaye.Alikuwa amelewa chakari wakati Makata alimpigia mwanawe simu aje kumchukua.Alihofia huenda akapatana na ajali barabarani iwapo angeamua kurudi nyumbani.Au hakutaka aage dunia na deni yake?John alikuwa na mawazo chungu mzima kumwona baba yake akiwa katika hali ile.Hajawahi kumwona baba yake akiwa mlevi maishani mwake manake alichukia ulevi.Isitoshe,alikuwa kasisi msaidizi katika kanisa moja la Kianglikana.
Alipomfikisha nyumbani alinga'anga'ana kumshusha garini na kumpeleka kitandani taratibu.Kinywa chake cha nasaha na busara kilikuwa kimegeuka na kuwa karakana ya matusi aina ainati.Mkewe alisimama kwa mshangao na kumsaidia John kumpandisha Matani vipagoni lama kitandani.John alimwangalia mamake kwa huzuni na babake kwa uso wenye maswali mengi.
“Goodnight mum.”Alisema kisha akaondoka kabla mamake hajamjibu.
'ukweli utadhihiri karibuni' John alikuwa akiwaza.Ulikuwa mwendo wa saa tatu na nusu hivi za usiku wakati John aliamua kujaribu kufukua ukweli wa mambo.Alikaa pale sebuleni hadi alipomwona mamake akitoka katika chumba chao cha kulala kwenda kufukuza uchovu bafuni.Ghafla akakimbia kwa kunyatianyatia ili asifanye sauti yoyote na kuufungua mlango taratibu.Akaelekea alipokuwa babake na kuingia mfukoni mwa kizibao chake,akatoa simu yake na kuchukua kidole chake cha gumba na kukitia katika sehemu ya nyuma ya simu ili ifunguke kwani ndicho kilichokuwa nywila yake.Alipofanikiwa aliufunga mlango na kwenda hadi chumbani mwake.Alipitia simu alizopigiwa kujaribu kuona kama angepata nambari yoyote ya siri ambayo huenda ilimsumbua kimawazo bila kufanikiwa.Akapitia jumbe alizopokea kutoka kwa laini yake ya simu,lakini wapi!Hakupata kitu.Mwishowe aliamua kuingia katika mtandao wake wa kunani (whatsapp) kusoma jumbe zake na kwa bahati akhiyari,akapata alichokuwa akinuia!.Ujumbe wenye mshiko na mnato na woga wa aina yake.
Alisoma;
'Nina habari kuwa wewe ndiye mkuu wa habari na uhariri katika runinga ya Leo.Kuna habari kuhusu Katega uliyoipeperusha Jumamosi kuhusu uagizaji wa dawa za kulevya.Sasa kuko hivi,tutatuma mtu huko kuja kuomba kazi ya uhandisi na uhakikishe kuwa ameipata.Pili,baadaye tunataka ujiuzulu katika kazi hiyo haraka iwezekanavyo.Tatu,utupatie jina la mwanahabari aliyerekodi kanda hiyo na kuiwasilisha kwako.Ukifeli kufanya hivyo,John,mtoto wako wa mwaka wa pili katika chuo cha Songa tutamuua,Makata,rafiki yako wa karibu auzaye bia tutamuua,mkeo wa miaka ishirini na minne tutamchukua katika jumba lake la nguo la kumuua,nyanya yako aliye kijijini katika eneo la Taka tutamchukua.Nne,Be a good boy and decide.'John alifikicha macho yake ambayo tayari yalikuwa yameanza kushamiri machozi yaliyotishia kuanguka.Hakuamini alipoona kuwa babake aliandika jina 'Opondo' na kueleza kuwa yeye ndiye aliyeleta kanda hiyo ya video.Iweje baba amsaliti kakake wa tumbo moja?Kwani ya wahenga kuwa damu ni mzito kuliko maji hayatumiki wakati wote?Yote hayo,ingekuwa ni wewe ungefanyaje ilhali mwenye kutuma ujumbe huo anajua kila kitu kuihusu aila yako?Kilichokuwa kikimkata maini sasa ni kuwaza hatua atakayoichukua ili kumfukua na kumfichua mwenye ujumbe huo.
Asubuhi yake John alienda na kuitupa simu ya babake garini baada ya kupiga picha ujumbe huo na kuichukua nambari husika ya simu.Babake alipoamka na kujaribu kuitafuta simu yake bila mafanikio,John akamwambia huenda iko garini.
John alishindwa achukue mkondo upi wa kutafuta ukweli wa mambo.Aende kwa Opondo au aamue kumuuliza babake ukweli wa mambo?Asemezane na Hadasa au akae kimya tu?Aliona ni heri aende moja kwa moja hadi kituo cha polisi akapige ripoti.“Baba,mwisho umeongea na Opondo ilikuwa lini?”John akauliza kama njia ya kujaribu kuona iwapo babake ataamua kusema ukweli.
“Samahani,Pengine ningeanza kwa kuwaomba msamaha kwa kile nilichofanya bila kuwajulisha.”John alitabasamu kisiri huku moyo ukimwenda kasi manake alijua wazi kuwa mawingu ya siri yataanuka asubuhi hii.Mamake alikuwa keshasogea karibu kumsikiliza.
Aliendelea,”Jana habari katika baadhi ya runinga zilikuwa kuhusu kakangu Opondo…”“Yuko salama?”John akadakia.
“Funga mdomo amalize anachosema kwanza.Utauliza maswali baadaye.Heshima yako I wapi?”
“Opondo alikunywa sumu na kujitoa uhai baada ya kumkatakata mkewe.”Matani alianza kulia na mabega kumchezamcheza.
“Audhubillahi mashetani!Opondo hawezi kufanya jambo kama hilo kama nimjuavyo.Ndoa yao hata haikuwa na doa.”
“Ni kweli lakini fahamu kuwa wakati mwingine ndoa huwa na siri kali,misukosuko hueza kutokea ghafla na kutanahabi,mastaajabu yanakodolea watu macho;kama haya ya sasa.”
“Kuna habari zozote kuhusu mtoto wao mdogo,Kamata?”Jesinta alikuwa akiuliza huku amemkumbatia mumewe na kukilaza kichwa chake kifuani pake kama mtoto mdogo ili kumliwaza.
“Nitaenda kuulizia majirani kule kuhusu Kamata.”John alikuli na kuondoka upesi.Hakutarajia babake angesema hayo.Alidhania kuwa angezungumzia kuhusu kujiuzulu kwake kazini na wapendwa wake kutishiwa maisha kiasi kwamba akamsaliti kakake.
“Tukio hilo lilinipata ghafla nikashindwa kustahimili uchungu huo ndiposa nikajipata nikibugia vileo.”
“kifo ni hasidi mkuu,hujepa kilicho kilizuri.Isitoshe tunda njema halikawii mtini.”
“Heri ungeelewa ukweli wa mambo.”
Follow me on Twitter
@WeyeMatuko.Like and comment.
YOU ARE READING
KARATA YA MAHABA
Short StoryOpondo,Mwanahabari mpelelezi wa runinga ya Leo anarekodi kanda ya video kuonyesha Katega akishiriki biashara haramu ya dawa za kulevya.Asilolijua ni kuwa alikuwa akijichimbia kaburi kwa kujaribu kushindana na ndovu kunya. Utaweza kusaliti mtu umpend...