karata ya mahaba 4

7 0 0
                                    

John alifika katika makazi ya Opondo na kupata wanapolisi wangali wamezingira jumba hilo ili kufanya upelelezi zaidi.Alitupa macho kujaribu kuona iwapo angeona mtu wanayehusiana naye karibu ili kuulizia kuhusu mwanawe Opondo.Bila kutarajia,akahisi mtu akimwita toka nyuma yake na kustaajabu alikuwa Hadasa.

“Makiwa.”Hadasa alisema.

“Tunayo.”John akajibu kisha akauliza,”Ulijuaje kuhusu tukio hili?Au mbona uko hapa?”

“Niliona kwenye habari jana Usiku,nikajaribu kukupigia simu na kukutumia jumbe bila mafanikio.”

“Simu yangu ilikuwa imezima,”John alijaribu kudanganya.

“Ilizima tangu utoke Bustani ya Anasa au ulinizuia kukupigia na kupokea jumbe zangu?”

“Tusiende hapo tafadhali.Nina mengi akilini.Nimekuja kujaribu kumtafuta Kamata kwa kuulizia majirani.”

“Najua aliko.Nilimwona akichukuliwa na wanapolisi na huenda wanangojea jamaa zake ili wawakabidhi.”

“Ahsante.”John alikuli kisha akaanza kuchukua misamba mirefu kwa upesi kwenda katika kituo cha polisi kilichokuwa karibu.Itakuwa kama kupata ndege wawili kwa jiwe moja;kukabidhiwa kamata na kuripoti kisa cha babake kutishiwa uhai na kupeana ujumbe wenyewe pamoja na nambari ya simu.

“Nakufuata na si tafadhali,upende usipende.”

Hadasa walifuatana na John kama mtu na jibwa lake.Walitembea bila kusemezana kwa muda mrefu  huku kila mmoja wao akiwa katika bahari yake ya mawazo.Hadasa alielewa sababu ya John kukatiza uhusiano wao lakini hakuelewa mbona hakupigania upendo wao,hakuelewa mbona afikie kiwango cha kukataa hata kuzungumza naye hata kupitia jumbe za simu na kuonekana mwenye chuki na ukali kupita ukawaida wake.Upande mwingine,John alikuwa akiwaza jinsi atakavyowasilisha ujumbe ule kwa polisi kuhusu tishio la mauaji kwa babake,aliwaza jinsi atakavyomwambia Hadasa kuwa ni bora wakae mbali na kila mmoja wao,aliwaza kama kuna ukweli wowote kutoka kwa maneno ya mamake kuwa Opondo hangefanya ukatili kama ule kwa mkewe.Alikuwa na mwao kuwa baba yake kunywa pombe ilikuwa njia ya kujitenga na ukweli kuwa yeye ndiye chanzo cha kifo cha kakake.

“Umewahi peleka kesi yoyote kwenye kituo cha polisi?John alivunja kimya.

“Hapana,mbona ukauliza vile lakini?”
“Si neno.”

“Si neno kiaje?Iweje ukauliza swali kama hilo wakati ambapo tunaelekea kwenye kituo cha polisi?”

“Hata nikikuambia sitafaidi kitu.”

“Nijaribu,”Hadasa alimwambia na kumkazia macho.Kando yao wakaona duka dogo wakaamua kwenda kukonga kiu yao.Wakaagiza soda na kuketi nyasini kwenye kivuli cha mti.Hadasa alikuwa bado na hisia za mapenzi kwa John.Alipendezwa na hulka zake na sauti  nzito.Urefu wake kama mlingoti na  uso wa kupendeza daima ulimfanya atake kuwa naye milele hata siku ya kiama.

“Natumai unakumbuka nikikuonyesha jumbe za Abdul kunitishia maisha.”

“Ndiyo nakumbuka.Waenda kumripoti?”
“Hata sijafikiria hivyo.Babangu alipata ujumbe wa kutisha zaidi na ndiposa naona ni vyema kuvunja kimya chake.”

“Una ushahidi wa kutosha kuhusu unachosema?”

“Huu hapa.”

Hadasa alisoma ujumbe ule na kukodoa macho.Akainua macho yake na kumwangalia John kama mtu aliyetaka kusema jambo baada ya kuona nambari ile ya simu.Aliikumbuka Vizuri sana na alijua ilitoka kwa nani.Miaka minne iliyopita alikuwa katika uhusiano mwingine na Degrada.Walijuana naye alipokuja kumtembelea  Abdul na haikuwachukua muda kabla hawajatiana machoni kisha moyoni.Kilichomvutia Hadasa kwa Degrada ni kuwa alikuwa mjuzi wa mambo mengi kando na misuli yake iliyomchukua sambamba na kumwacha kama  mwanabondia.Walikiri kupendana na kucheza na kutalii sehemu nyingi za raha na kucheza densi pamoja na kushiriki tendo la ndoa si mara moja wala mbili.Walishibana kusema tosha hadi wakati mmoja Hadasa alipomfumania Degrada akishiriki ngono na Naomi,rafiki yake wa karibu.Nambari ile ya simu ilimkumbusha mbali na kumjaza hasira na dharau moyoni.

“Najua mwenye nambari hii ya simu.”
“Wamjua?Ni nani haswa?”John hakuonekana kuamini maneno ya Hadasa.

“Alikuwa mpenzi wangu wa kitambo lakini tukatengana.Ni rafiki wa karibu wa Abdul.”Hadasa aligutuka baada ya kutaja uhusiano wa Degrada na Abdul.Akajua wazi kuwa ameshamtia ndugu yake kikaangoni akabakia kujihukumu nafsini.Enga kabla ya kujenga.

“Kuna uwezekano mkubwa ndugu yako alihusika manake ujumbe huo ulitaja baba yako.”

“Huenda lakini hatuna uhakika.Sijawahi kumwona na ndugu yangu tena tangu tutokane.”

“Hadasa,najua unampenda ndugu yako ila huoni kuna usawa wa kutishiana maisha baina ya ndugu yako na mpenzi wako?”

“Si mpenzi wangu,anaitwa Degrada.”Hadasa alikosoa kisha akaendelea,”John nakuomba usimhusishe Abdul na chochote manake nilishaongea naye na akaomba msamaha.”

“Alikuomba msamaha ila si mimi.Mbona nimfiche fisi?Wewe huoni kuwa swala hili ni nyeti sana?Isitoshe,Kifo cha Opondo si fumbo hata kidogo,Degrada au Abdul au babako ana uhusiano nacho.Huoni sababu ya babangu kujiuzulu kazi na kuhakikisha kuwa kuna mhandisi mgeni katika runinga ya Leo?Huoni uhusiano wowote wa kanda za video kupotea kabisa baada ya baba kujiuzulu na baada ya kifo cha Opondo?”

Hadasa alikaa pale tutwe asiseme kitu.Mtima ulimtuturika na ulimi kutetereka asiweze kuongea vizuri.Ni kweli kuna uhusiano fulani wa yote aliyosema John lakini hakutaka chochote kibaya kimfike ndugu au baba yake.Wote hawa walikuwa waamba ngoma ambapo kila mmoja anavutia kwake.

“Hadasa,ninachofanya si ubinafsi bali ninafanya kinachostahili kufanywa.Nikimficha fisi leo,kesho atanigueza kitoweo.”

John alilipia soda walizokunywa na kuanza kufululiza tena mpaka kituo cha polisi cha Haki Tena.Hadasa Alimfuata ingawa shingo mkingamo.Alijua Abdul na babake watakuwa katika kesi nyingine ambayo huenda ikawa muhali kujitoa.

“Mimi ni jamaa ya Opondo na nimepata habari kuwa mtoto wake yuko mikononi mwenu.”

“Tutadhibitishaje?Wajua hatuwezi kupatia mtoto kiholela halafu tupate habari kuwa ulituongopea.”

“Hiki  hapa kitambulisho changu cha taifa pamoja na nambari yangu ya simu.Zaidi ya hayo mtoto ananijua kwa sura na majina.”

Askari aliyekuwa pale alimwangalia John na kumgeukia Hadasa kwa kumchuja kisha akaamuru Kamata aletwe.Kama alivyotarajia,kamata alimkimbilia John na kubebwa juu juu.

“Mum na Dad watarudi?”Kamata aliuliza kinyonge.

“Nimekununulia maziwa na keki tamu.Tukitoka hapa nitakupatia.”John alijaribu kulikwepa swali la Kamata kwa mafanikio.Lakini je,ataishi kulikwepa hadi lini?Hadasa alihisi kulia haswa aliposikia Kamata akiuliza kuhusu wazazi wake.Alijiita mkutano nafsini mwake na kuamua liwalo na liwe angemsaidia John kuhakikisha haki imepatikana hata ikiwa ni aila yake kutiwa nguvuni.

Alipiga moyo konde na kumwambia John,”Nipe mtoto nikacheze naye pale nje.Ripoti tukio hilo.”

Hadasa alimchukua Kamata na kumwonea imani sana.Mtoto mdogo ambaye huenda alipokonywa wazazi wake wawili kikatili na kuachwa yatima atalazimika kuishi kwa maswali kuhusiana na wazazi wake mpaka achoke kuwaulizia.Swala hili halikumkaa wazi akilini asilani.Baada ya Muda wa takriban dakika thelathini,John alitoka akiwa na matumaini kuwa haki itachukua mkondo wake na waliohusika kuwindwa na kutupwa gerezani.Alimkaribia Hadasa na kumkumbatia na kumpa busu la shavuni kama ishara ya kupendezwa na ujasiri wake. Walipoondoka,askari mmoja kati ya watatu waliokuwa pale kwenye zamu kurekodi na kuchukua picha za ujumbe ambao John aliwasilisha aliondoka kisiri na kwenda chembani kupiga simu.

“Hello Abdul,Kamwambie Katega kuwa mambo hayajalainika bado.Dada yako,Hadasa na mvulana aliyejitambulisha kama John wamewasilisha ushahidi ambao nahofia ni vigumu kuutoroka wakati huu dhidi ya Degrada  kuhusu ujumbe aliomtumia Bwana Matani.”

KARATA YA MAHABAWhere stories live. Discover now