Sura ya Saba

22 1 0
                                    

Baada ya kupewa cheti cha siha njema, Suzzanna aliondoka hospitalini akiwa buheri wa afya.
Hata hivyo,kama alivyopanga Jason alionelea,na kusisitiziwa na jamaa zake kuelekea kule Marekani kwa uchunguzi zaidi.
Akawa ameifunga safari kuelekea Marekani na kuishi maskanini kwa rafikiye,Jason.
Lopezi alikuwa mke rasmi wa Jason na walijaliwa wana wawili wa kiume.
Lopezi alikuwa mwanamke mrembo na asiyetaka dhihaka kwa mumewe.
Alimlinda Jason jinsi simba awalindavyo majike katika familia yake.
Alifahamu fika kuwepo kwa mabanati  wachuna wasikopanda ambao walijitwika jukumu la kuwafuata wachezaji waliobobea wakiwadai kushiriki mapenzi haramu nao.
Mwanzoni mwa ndoa yao, Lopezi alimfuata mumewe kila alipoelekea ukumbini kwa mazoezi au kucheza.
Hata hivyo,muda ulivyosonga na hasa baada ya kuwapata wana, ilimbidi kupunguza safari zake za kushika doria na kumwacha mumewe kujichunga mwenyewe.
Kuna wakati alimwambia Jason kuwa alikuwa amemruhusu kudonadona nje ya ndoa,lakini asizindishe mara mbili kwa mwaka.
Kauli hii ilimwacha Jason amepigwa butwaa asijiue kama ilikuwa fursa ya kuku kufunguliwa kamba mguuni au kilikuwa kipande cha nyama kwenye nduano kumkamatia nyangumi.
Kila alipokumbana na mabanati hao; wengine wakijirusha nusu uchi mbele yake,na hata kuingia vyumba vyake vya kupumzika kisiri,aliyakumbuka maneno ya mkewe na kujinasua.
Kwa sasa hofu ya Lopezi ilikuwa imepungua kiasi cha haja kwa kuwa Jason alikuwa na walinzi waliomfuata kila alikokoenda na kumkinga kutokana na umati wa aina yoyote.

Jason hakuwa anataka mafarakano au tuhuma zozote pale kwake nyumbani,kwa hivyo alipanga na Suzzanna kuwa,akiwa kule Marekani angeigiza kuwa binamu wake.
Mpango huu ungemwepushia Suzzanna makali ya Lopezi.

Baada ya kuwasili salama salmin, Suzzanna  alikwenda hospitalini na kudhibitishwa kuwa mzima kama kigongo.

Suzzanna alibaki na muda wa takriban majuma mawili, kutembea na kuyaona kwa macho mawili maisha ya ulimengu wa kwanza.
Maisha ambayo hapo mbeleni aliyaonea katika runinga na sinema.
Maisha kule Marekani yalikuwa maisha ya kasi zaidi akilinganisha na nyumbani Afrika.
Miundo msingi kule ,ilikuwa imeundwa ikaundika.
Mbinu za uchukuzi zilikuwa zikiendeshwa kwa mitambo ya tarakrishi na uratibu  wa kushangaza.
Hakuwahi kushuhudia misongamano ya magari barabarani.
Uchukuzi wa umma ulitegemea sana huduma za magari moshi ya kisasa.
Ilikuwa rahisi kukadiria na kupanga muda wa kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Usafi katika miji ulikuwa wa kimbinguni.
Kwa kuzoea mirundikano ya taka nyumbani,alipata picha ya ahela kutakavyokuwa siku yake ya kiama ikifika.
La kushangaza zaidi ni kuona jinsi mito yenye maji safi ilivyopita katikati au kuizungaka miji na kuiacha na vijipepo vya kubarizia.
Majengo yalipangana kama meno kwenye ufizi huku miti na maua yakipandwa kwenye njia na vijia vyote.
Kulipendeza kama bustani kwa malkia.
Kila barabara ilikuwa na sehemu ya wapita njia,magari na waendesha baiskeli.
Kulikuwa na sehemu za wenyeji kukutana na kupumzika katika kila mji.
Suzzanna aliungama na picha viichorayo vyombo vya habari vya magharibi kuwa,maisha Afrika ni 'maisha ya zogo na kuchanganyikiwa'
Asiyeonja chakula kwingineko huishi daima kuamini kuwa mamake ndiye mpishi hodari kabisa duniani, Lakini kumbe wapo wapishi bora na shupavu zaidi!

Afrika majumba hujengwa bila utaratibu wowote,na kujazana sehemu zozote zilizo wazi.
Si ajabu kupata majumba yaliyojengwa juu ya mito au juu ya vidimbwi vya maji.
Afrika miti miti hukatwa kujengea majumba mabovumabovu yanayobomokabomoka kila mara,nyuma yakiacha vifo na vilio.
Afrika uchafu ndio usafi mijini.
Badala ya mito huwa vijia vya kupitishia maji taka yaliyojaa kila aina ya vifurushi na kemikali.
Maji si maji bali mchanganyiko wa aina ya taka na kemikali mbalimbali zonayapaka mchanganyiko wa rangi ja kinyonga
Kuisafisha miji ya Afrika kulihitaji kusafisha akili za Waafrika wenyewe?

************************************
Kila chenye uzuri hakikosi kasoro.
Marekani,Suzzanna alikumbuna na saratani ya ubaguzi wa rangi kimasomaso.
Lopezi alikuwa amemuomba kuandamana naye kwenda kununua nguo na bidhaa nyinginezo za upodozi.
Waliipoingia katika duka moja la nguo,walikosa wa kuwahudumia na wakaambiwa hawangezimudu bei za pale.
Wahudumu wote walikuwa wazungu weupe,warefu kama twiga.
Lopezi aliwachoma wahudumu wa duka lile kwa moto wa ulimi hadi wakawaita polisi kuwafurusha nje.
Suzzanna alijipata taabani kwa kutakiwa kuonyesha stakabadhi kudhibitisha kuwa alikuwa kule Marekani kihalali.
Mibaba ya polisi iliwatega na kuwaangusha chini tayari kuwatia pingu lakini, waliwaachilia wakati vurumai lililokuwa likiendelea kuwavutia wapita njia, waliowazomea na kutishia kuchoma duka lile.
Hapo ndipo Suzzanna alitamani maisha duni na ya hobelahobela lakini matulivu ya Afrika.
Tukio la pili lilitukia wakati Suzzanna akiandamana na Jason ukumbini kutizama mechi ya ligi kuu ya vikapu Marekani.
Suzzanna aliketi karibu na vitoto vichokozi vilivyo mdonadona kuona kama vidole vyao vingebaki na matone ya rangi nyeusi.
Kuna kivulana kichokozi kilichomwigizia Suzzanna visura huku kikitoa sauti za nyani.
Kingine kilijilazimisha kunyamba na kuwachilia mripuko wa harufu iliyowaacha mashabiki wakishika pua  na kujipepetea upepo.
Kilimusingizia Suzzanna.
Alitamani kukimeza kizomakizima amezavyo chatu,lakini akaogopa kuitiwa polisi.
Tukio la tatu lilitokea, siku akiabiri gari moshi,ambapo mwanaume mbaguzi alimkamata maziwa na kuufinyia uume wake kwenye makalio ya Suzzanna.
Kwa dume hili ilikuwa sarakasi iliyowaacha wenzake wakiangua kicheko.
Suzzanna alikusanya nguvu zake zote na kukiezeka kinyangarika hicho,kofi lililokiacha kikiona vimulimuli na kuwaacha wenzake wametulia tuli kama maji mtungini,kwa uoga.
Suzzanna alishangaliwa na kupigiwa makofi na abiria wenzake wanawake.
Licha ya matukio haya Suzzanna akikubali kuwa,'kipya kinyemi kingawa kidonda'
Mgeni siku ya kwanza mkaribishe wali.
Mgeni siku ya pili mkaribishe mkeka alalie.
Mgeni siku ya tatu mtembeze ajionee mageni.
Mgeni siku ya nne mpe jembe akulime.
Mgeni siku ya tano muage arudi kwao.
Siku ya tano kwa Suzzanna ilikuwa imefika na hakuwa na budi ila kuabiri ndege kurejea kwao nyumbani kuendelea na masomo yake.
***********************************
Yaliyowatukia watoto wa Mathangi yaliwaacha na mahangaiko si haba, na ya kiakili yaliyohitaji usaidizi wa washauri wa kisaikolojia.
Bundi alijitwika jukumu la kuambatana na malaika hawa wa mungu katika kuwapa ushauri akishirikiana na wataalam katika shirika lao lisilokuwa la kiserikali,'Mental Health Afrika'

Watoto wlioadhirika kimawazo kutokana na sababu moja ama nyingine huweza kulemaa katika kukuwa kwao.
Wengine huanza kuwa na hamaki na kuwa watundu au wakaidi.
Kuna wale hushindwa kuvumilia mazingira yanayowatatiza kisaikolojia na kukimbilia mitaani.
Hawa ndio baadhi ya wale wanaishi vishororoni,kwa kawaida wakiitwa, 'chokora matangi'
Ni wana wakamilifu kama wengine walio manyumbani, ila wanalazimika kuchokora mapipa ili kujipatia tonge wasife njaa.
Iwapo utachukua muda wa kuzungumza na watoto wale wanaoranda mitaani,utafahamu ni watoto wenye azima na ndoto za kimaisha kama watoto wengine wowote wale.
Ndoa zinazoyumba huwa na madhara zaidi kwa mtoto wa kike kuliko wa kiume.
Mtoto msichana alelewapo bila mapenzi ya wazazi wote wawili,anapobarehe,hujiingiza katika mahusiano na wanaume huku akitafuta nafasi aliyoikosa ya kupendwa na wazazi.
Mahusiano haya huishia katika mimba za mapema,ukahaba na kuavya mimba.
Mtoto akosapo uelekezi wa kimaisha na mapenzi dhabiti ya wazazi, hujiingiza katika utandu wa madawa ya kulevya,wizi na maovu mengine.
Kwa hivyo ni vizuri kuwashauri na kuwaonyesha upendo watoto wanaojipata katika mashaka kutokana na maamuzi mabaya ya wazazi wao.
Watoto wa Mathangi walibahatika kuwa na wendani,na mama mzazi aliyejitolea kikondoo kuhakikisha maisha yao yalisonga mbele na kurejea hali timamu.
Walijiunga na shule yao mpya ya 'Tumaini Academy'  na kuendelea na masomo yao.

************************************
Wakati wa Bundi kurejelea masomo yake ulikuwa umewadia.
Alijiunga na chuo alichokuwa mpenziwe, Suzzanna,na kuyaanza masomo mapya ya saikolojia na ushauri,huku akiendeleza kampeni yao ya 'afya ya kiakili' kama zamani.
Chris na Rosata walishikamana na kurejelea uhusiano wao wa zamani.
Wakawa chanda na pete na kugandana kama kumbikumbi watokeapo viotani mwao na kuyavua mabawa,wasiruke tena ila kuandamana sakafuni.

Wahadhiri midume ya  'alama za ngono' ilipigwa kalamu na mingine kujitorosha yenyewe kwa fedhea na aibu.

Jina Suzzanna lilikuwa limeandikika katika nyoyo na vitabu vya kihistiria, kwa kuleta mabadiliko,sio tu chuoni mwake, bali kakita vyuo vingi duniani.

Ilitarajiwa pia kuwa waajiri wangebadili maono yao na kuwa na imani na vyeti vya waliofuzu kutoka vyuo hivyo.
Suzzanna alishamiri,akahojiwa na vyombo tofauti tofauti vya habari na hata kutunukiwa taji la ukakamavu na rais wa taifa lake.
Chanda chema bila shaka huvishwa pete!

SUZANNAWhere stories live. Discover now