Nlijisetiri kwenye kibanda cha msonge kilichokua kimechakaa mwishoni mwa jiji. Mawazo mengi yalinikaba ila majibu hayakuwepo kati yao nlishindwa kwa nini maisha yalikua yakinipeleka mbio kiasi hiki
Kuna muda ndoto na fikra za kujiua zilinijia ila nilikua na imani iliyozidi fikra. Kunguni waliokuwa kwenye chumba hiki chakavu hawangekupa ruhusa ya kumuita mja maskini. Maji upande huu wa jiji yalikuwa kama maziwa ya kuku wa kiluhya sikuwa na jingine ila kuvumilia hili lililonisibu
Halua alikuwa mwanamke mmoja nliyetaka kuwa na yeye maishani.Sijui kwa nini kwa muda mfupi nliomjua aliyageuza maisha yangu kabisa na kunipa mtazamo mpya kwa wanawake na mapenzi. Zipo nyakati nikiwa kwenye mahame haya nliyoyaita kwangu nlitaka kutunga shairi ila maneno yakanikosa maana kila mara nikifikiria utenzi picha ya halua ilinijia machoni.
Jioni moja nikiwa naruka mitaro ya maji taka kuelekea kwangu toka hangaiko la siku nlikutana na muujiza.Gari la Halua lilikua maegezoni na kando yake kasimama yeye na watoto wawili walokua wanajisetiri kwenye kibanda kilichokua mkabala na changu.Wavulana hao waliniona na kunielekezea vidole wakiniashiria. Nlijua kingejiri kitendawili hivyo nlijilaza chali kando ya jaa lililojaa taka na uvundo mkali na kujivuta chini kama joka la mdimu .
Walipofika walikoniona nami nlikua tayari nishaingia kwenye umati wa sokohuru na kutokomea.Siku hiyo niliamua kuhama na kuenda mbali tena mahali ambako singepatwa na Halua.Huyu mwanamke alikua zimwi au mzuka maana asubuhi nlipokuwa nafunganya virago vyangu mlango ulibishwa. Nlipofungua sikuamini macho yangu. Halua! na urembo wake wote alikua kasimama pale kama nyota iliyotumwa kuangaza chumba kile.
Sikua na lingine ila kumkaribisha sebuleni au tuseme kule nlikokubandika jina sebuleni. Aliniangalia machoni kisha akaanza kudondokwa na machozi pindi tu alipoona hali ya chumba kile. "Mbona uliondoka kwangu?mbona ulinihepa kwenye siku muhimu mpenzi? Yale yalikua maneno ya wazazi wangu na nlishawakanya wasiingilie tena maisha yangu kiasi hicho." Alianza kuongea huku akidondokwa na machozi .
Mimi nlisimama tu pale langoni nikimwangalia kama bubu aliyekutana na mkombozi."Tangu uondoke nami sijakaa kwangu, nlidhani umeenda pale nlipokuokota siku ile lakini nilipofika nikapata kukavu.Sijui mbona umeamua kunyamaza na kujificha tusionane tena. Mimi mpenzi sina ubaya tafadhali rudi kwetu tuishi na raha" aliendelea kusema
"Sitaki unikumbushe yaliyojiri siku hiyo.Nishayasahau mimi, nishawasamehe wazazi wako maana wana kila sababu ya kunisuta na kunichuja kama walivyofanya.Napenda maisha haya ninayoishi maana kama mchochole nafaa tu kutangamana na wachochole.Na kuhusu ombi la kurudi nyumbani kwako hilo haliwezekani maana mimi nishaamua kukaa huku na kujitafutia kipato changu huku na ijapo siku njema basi nyota yangu itang'aa" Nlimjibu.
Aliniangalia tena na mara hii macho yake yalijaa huruma, hasira , upole ,kukosa imani na kila mseto wa hisia. Nlipofungua kinywa alinyanyuka kule alikokua kaketi na kunikaribia kisha akanishika bega kama alivyoishi kufanya kila alipotaka nimfanyie jambo hili au lile. Nlijua akiwa karibu hivi sikuwa na jingine kwa hivyo alishinda kesi yake ya kunirudisha kwake na kunitunza kama mume
YOU ARE READING
Ipo Siku
HumorWosia wa babu yangu ukitimia naapa nitakua mtu asiye na kiburi.Naapa kutimiza yote aliyoninongonezea na ninaapa kuitunza aila yangu bila kiburi wala dharau. Maana natumai IPO SIKU.