Episode 1

136 7 2
                                    

"Tadi usilale, laaala laaala,
Tadi usilaleee,
Bado mapambano,
Baaado mapambano, bado mapambano”
Kipaza sauti kilipaaza uwanjani Takia. Umati wa watu ulionekana ukifululiza uwanjani ambako kulitokea sauti.

Sauti ya Fahama Makumbo iliendelea kuhanikiza hewa ya mji wa Takia.
“Sisi hatutishwi na chocha za wapinzani wetu. Wale ni Kama matawi ya mti ambayo wakati wa masika hutokea na kushitadi ilhali hunyauka na kupukutika wakati wa kiangazi.” Makofi, vifijo na nderemo vilifuatia usemi wake.

“Nyinyi nyote mwamfahamu Bwana Tadi Makumbo Kama mwanasiasa tajika.” Aliendelea Fahama.” Anayo maono makuu yanayoweza kutimiza ruwaza ya mji huu .” Alizidi kummiminia sifa huku umati ukishangilia kwa mihemko.

Mheshimiwa Tadi Makumbo alikuwa mmoja kati ya wanasiasa watano waliopania kutwaa kiti cha uongozi cha mji wa Takia. Alikuwa mwanasiasa mkongwe mwenye tajriba na haikuwa mara yake ya kwanza kujitosa ulingoni; ila mara yake ya sita. Ila katika kujaribu kwake huko, hakupata kuongoza Takia. Hata hivyo, hakukata tamaa akijua fika ,’ mvumilivu hula mbivu’.

Kila baada ya miaka mitano alijitokeza na sera sufufu. Watu walimuenzi. Wengi walimpigia kura. Wakasema ‘wakati wetu ndio huu’ ila azma yao haikuwahi kuja kutimia.

Je, ni watu walimpiga mafamba wakati wa kampeni na kutompigia kura uchaguzini? Au ni sera zake hazikutosha kumfikisha alikonuia? Ama ni wapinzani wake waliompoka kura? Yakini, haya ni maswali ambayo hayakukosa kumpitikia Tadi na wandani wake wa kisiasa.

Tadi aliketi ndani ya gari lake la thamani lililonunuliwa kwa ‘pesa za wananchi’ kama walivyosema wasemao. Moyo ulimpapa pale dereva wake alipolitia gari moto kuelekea uwanja wa Takia. Ilikuwa Siku nyingine-Kama ilivyokuwa ada yake-kuorodhesha tena sera zake atakazotimiza ikiwa atachaguliwa. Alijua bayana kuwa upinzani aliokuwa nayo ulikuwa mkali hasa kutoka kwa Bwana Mtanzi Matambo.

Itaendelea

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now