Episode 33

7 1 0
                                    

Aliyapangusa machozi yale kwa kiganja chake kilichokuwa tayari kinatetemeka kwa woga.
Aliutazama upanga ule kwa muda. Ulikuwa ukichonyota mithili ya kile kisu alicholekezewa shingoni na Mhazili usiku ule wa kutekwa nyara kwake. Machozi yalilowesha shati lile
alilokuwa amelivaa na lililokuwa limechanikachanika kwa kuvutwavutwa na Mhazili.

Mariko aliuelekeza upanga ule kifuani mwake huku machozi zaidi yakimpukutika machoni wake. Mara alianza kujizungumzia mwenyewe kwa uchungu.
"Sikujua kuwa maisha yangu yatageuka na kuwa yasiyotamanika kuishi. Sikujua kuwa kuna siku nitashikwa mateka sababu ya kutaka kufyeka njia ya haki iliyoachwa ikamea magugu na
kufunikwa na msitu. Sikufahamu kuwa ari hii ya kutaka kuleta mageuzi mjini Takia ungenifikisha huku. Kuigharimu familia yangu furaha yake. Haki imebanangwa kote. Si ofisi ya kiongozi mkuu wa Takia, si mahakamani, si wanapolisi wenyewe, si idara yaupelelezi; takribani kila idara imeambukizwa ugonjwa wa Mtanzi. Afadhali mimi mwenyewe nijimalize kabla wao hawajanimaliza wenyewe..." alisita ghafla. Akachukua hatua kadhaa na kuketi kochini angali
ameuelekeza upanga ule kifuani mwake. Akanyanyuka tena na kuelekea pale palipokuwa
runinga ile. Akasita kabla ya kuibonyeza.

Fikira ya kuwa na mke na mwana ukamsimanga hadi akaghairi nia ya kujitoa uhai. Alifahamu
fika jitimai ambayo wangekuwa nayo wakifahamu kuuka kwake. Aliibonyeza runinga ile na picha aliyoiona ilimfanya kushikwa na kinyaa. Matata Masumbufu ndiye aliyekuwa akimulikwa akifika shuleni pale kupiga kura yake. Alilakiwa na Mtanzi kwa bashasha kuu.
"Mama yangu wee!" Mariko alijipata katamka. "Mtanzi na Matata?! Viongozi wa Takia? Tutaishi kwa matata kweli hadi tujitie kitanzi. Huyu siye Matata ambaye juzi kahukumiwa kwa kupatikana na hatia ya kupoka familia ya bwana Haidara shamba lao? Si ni Matata ambaye fedha nyingi mno zilipotea alipokuwa waziri wa fedha katika serikali hii ya Mtanzi? Ndiye huyu hatua chache tu kuwa wa pili katika uongozi wa Takia?" Mariko alijisaili kimoyomoyo.

"Matata! Mataa-ta! Matataaa! Mraibu na mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya. Mara ngapi amepatikana
bila yeye kufunguliwa mashtaka? Sasa nafahamu sababu ya uhuru wake. Mtanzi!"

Mariko alijawa na hasira. Alitoka shoti na kuupiga mlango ule teke. Akaurusha upanga ule chini.
Alitaka atoke aende aichukie familia yake na atokomee popote pasipokuwa Takia. Mradi awe mbali na uongozi huu wa Mtanzi na Matata. Sasa aliona jahazi la Takia likizama taratibu pasipo yeyote aliye na uwezo wa kuliokoa. Giza liliingia huku matumaini ya Mariko yakiendelea
kudidimia taratibu. Alishusha pumzi kwa nguvu na kujirusha kochini. Uchovu, simanzi na njaa
ilimwia vigumu kuhimili na alihisi usingizi mzito ukimparamia licha ya kuwa na hamu kuu ya kujua ni nani atakayeibuka mshindi katika uchaguzi huo. Usingizi mzito ulimwiba na akalala fofofo!

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now