Episode 4

38 4 2
                                    

Inaendelea….

SURA YA PILI

“Hali hii ya kisiasa wafikiria hatima yake ni nini?” Katu alimsaili Karisa.
“Ndiyo hali tu ya kisiasa, mambo huenda yakatulia hivi karibuni.” Karisa aliliwaza.
“Hali gani? Wajua kushutumiana huku ni hatari kwa usalama wa mji huu?!”
“Kila mwamba ngoma huvutia kwake.”
“Basi wavute kwa uadilifu.”
“Uadilifu katika siasa?! Uadilifu ni kitu cha mwisho kitawahi kuwako moyoni mwa mwanasiasa hasa huku Takia.” Karisa alikaulisha.
“Mimi binafsi siwapendi wanasiasa wengine hasa huyu Mtanzi.” Aliendelea Karisa. “Sijui vipi Wanatakia walimchagua kipindi kile kilichopita. Sasa anatughilibu kwa pesa ili kutughalifisha yaliyopita. Mbona wanamji huu wasifunguke macho?”
“Hapo hapo mwenzangu. Ndiposa nakuuliza waonaje hatima yake?” Katu alirudia kusaili.
“Hali ni tete.”
“Tete hadi inatetemesha.” Alicheka Katu.
“Hasa!” Alisema Karisa akipiga bongo zaidi. “Lakini Mtanzi ni wa aila yenu. Pasi na shaka mumefaidika sana na uongozi wake.”
“Ndiyo.” Katu alikubali. “Daima damu ni nzito kuliko maji.”
“Ahaa! Umewahi kujiuliza pesa hizo zote anazitoa wapi? Ni mara ngapi tumesikia pesa za umma zimetoweka? Uchunguzi unapofanyika huisha bila aliyeziiba kujulikana? Waona hizi ardhi zote anazomiliki Mtanzi? Wazijua zilikuwa za nani mwanzoni?
Sakata hizi unazozisikia ambazo zimezua maswali mengi kuliko majibu nani atazitatua? Ukweli u wapi?”
Mtanziko huu wa matukio ulimkumbusha Karisa kisa kimoja cha kutamausha.
*   *   *
Majanga yaliyoyafika aila yake bwana mmoja kwa jina Masumbuko yalikuwa ya ukatili usiomithilika.
Masumbuko na aila yake waliishi kijiji cha Kazitosha mjini Takia. Alikuwa mkongwe sana. Alikuwa na mke na wana wawili. Hakuwa masikini sana ila ‘wasitara hasumbuki wa mbili havai moja.’
Asubuhi moja mzee Masumbuko aliamkia makali ya tumbo na kifua asiweze hata kujinyanyua toka kitandani. Aila yake ikidhani yalikwa maumivu ya kawaida na yangetoweka, maumivu yale yalimzidi mzee Masumbuko. Haikupita muda mrefu Masumbuko akaiaga dunia. Soni iliyomkumba mkewe baada ya kuuka kwa Masumbuko haikuwa kidogo.
Siku ya maziko yake, watu walifurika nyumbani kwa Masumbuko kumpa mkono wa buriani. Basi maiti yake ilifukizwa mchanga huku wapendwa wake wakilia kwa mafadhaiko. Laiti wangalijua hayo hayakuwa machozi ya mwisho kwao kulia!
Majuma kadhaa baada ya kumzika mzee Masumbuko, familia ile ilijipata katika kisanga kingine cha kuatua moyo. Nusura wateketezwe nyumbani huko usiku wakilala. Sababu ya kuteketezwa kwa makao yao kikibaki kitendawili kisicho jibu. Waliotekekeza uovu huo wakidai kufuata amri kutoka kwa ‘mkubwa’. Aidha, walidai kuwa mzee Masumbuko alikuwa ameinadi kipande hicho cha ardhi kabla kukumbana na mauti yake.
Lo! Maskini mkewe Masumbuko hakuamini macho na masikio yake. Ama alidhani ni ndoto ambayo katu hakutaka kuamkia uhalisia wake au ni kisulisuli tu; macho na masikio yake yanamchezea shere. Hata hivyo, huu ulikuwa ukweli mchungu kwake. Lialia zake na watoto wake za kutafuta haki ziliambulia masikio ya uziwi. Walivyozidi kutafuta haki makortini ndivyo haki ulivyozidi kuwaambaa. Kila walipoenda kutafuta usaidizi hawakusikizwa. Walipogundua kuwa kwa mnyonge kupata ni kwa mwenye nguvu kupenda, wakaamua hawatopiga ngumi ukuta tena. Wakaambulia haidhuru ingawaje haidhuru hudhuru.
*      *      *
Karisa, kando na kuwa wachache wa watu walio na ushawishi mkubwa wanaoaminika, falsafa yake na maono yake yalikinzana pakubwa yale ya wakiokuwa uongozini. Ni wachache sana kama yeye walikuwa wamesalia mjini Takia. Wengine waliojihusisha katika kujaribu kuwausia umma kuona na kubatilisha ukatili uliokithiri mjini Takia ‘walionwa kando’.
Hata hivyo, aliamini kuwa ipo siku mtume atashuka kuwaauni toka mikono ya ukiritimba, ubadhirifu na manyanyaso.

Itaendelea…..

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now