Episode 30

9 3 0
                                    

Siku ya uchaguzi. Tadi kama kawaida yake aliandamana na mkewe Bi. Mterehemezi hadi kituo
cha kupigia kura cha shule ya Bahati. Hapo ndipo wagombezi wote walitarajiwa kupiga kura zao
siku ile. Tangia kupata mshtuko ule wa moyo ambao almanusura kumuua, mikutano mingi
alimtuma Fahama Makumbo kwa niaba yake.

Bi. Mterehemezi na mumewe walifika shuleni Bahati wakiwa wa kwanza ili kupiga kura yao. Walifika
na kukuta umati wa kwanza umefika kuwachagua viongozi wao. Wafuasi wao waliwaandama
nyuma huku wakiimba na kumshangilia Tadi kwa vifijo na nderemo. Alifanya hima maana alijua
kuwa muda mfupi ujao wafuasi wa Mtanzi wangefika na kuzua zogo.

Alikumbuka fika katika
uchaguzi uliopita ambao ulikumbwa na ghasia za baada ya uchaguzi pale wafuasi wake na wale wa
Mtanzi walipokabiliana vikali.

Alipokwisha kupiga kura yake, Tadi na mkewe waliondoka na
kuelekea nyumbani kusubiri matokeo huku Tadi akiwa na matumaini ya kumbwaga mpinzani
wake mkuu Mtanzi.

Picha za Mariko Sipondi zilizokuwa zimebandikwa kote hazikuwa na maana tena. Wagombeaji
wengine walipokuwa wakijimwaya ulingoni kupiga kura yao,yeye hakutokezea. Hii ilibaki kama
kumbukumbu chungu mioyoni mwa wafuasi wake wakuu. Wengi wa wafuasi wake hawakujitokeza kupiga kura. Walibaki makazini pao kungojea kuelekezwa tena katika miaka mingine mitano ya dhulma za kisiasa. Wimbi la simanzi lilikuwa sehemu ya siku hiyo ya uchaguzi hasa walipokumbuka kuwa kuna uwezekano kutoweka kwa Mariko ni sehemu ya kubanangwa haki yao.

Kwa upande mwingine, Mtanzi aliketi nyumbani kwake akifuatilia kwa karibu matukio ya
uchaguzi. Alinyanyuka toka sebuleni mwake ulipofika wakati wake kuelekea Bahati kujipigia
kura. Alivaa tabasamu akijua fika kuwa mpinzani wake aliyekuwa akimwogopeza sasa alikuwa
‘maiti’. Alijitoa nje kimasomaso huku wafuasi wake wakimngojea kwa hamu na hamumu.

Mhazili naye tayari alikuwa ameshafika nyumbani kwa Mtanzi tayari kuandamana naye. Licha
ya uchovu aliyokuwa nayo, hakutaka Mtanzi ashuku chochote. Mtanzi aliingia garini huku Mhazili anasinzia polepole. Aligutuka pale Mtanzi alipoanza kuzungumza.

“Unalala asubuhi wakati umeamka tu muda mchache uliopita?” Mtanzi alishangaa.

VUTA N'KUVUTE Où les histoires vivent. Découvrez maintenant