Episode 22

10 1 0
                                    

Inaendelea… 

Mtanzi alimtazama Mariko kwa hamu na wasiwasi pia. Matarajio yake yalikuwa makubwa kwani haikuwa mara yake ya kwanza kushawishi mtu ama kwa maneno au pesa. Mariko naye wakati huu wote alikuwa anawaza. Watu wengi walikuwa na imani kuu naye na hakuwa tayari kuisaliti imani hiyo. Hakuweza kukisia jinsi mkewe angezipokea habari hizo ikiwa atakubali kujiunga na Mtanzi. Alikuwa amewasikia wengi waliohaidiwa makuu ilimradi wajiunge na Mtanzi. Baada ya kukubali ndoa hiyo, wakanyanyaswa na kuvuliwa sera zao. Mwishowe wakawa vibaraka wa Mtanzi. Mariko hakuwa radhi.

“Wazo lako zuri.” Mariko alisema hatimaye. “Lakini mimi sina nia ya kuungana na mtu yeyote. Ninaamini ninao wafuasi tosha na malengo yangu katu hayaambatani na yenu. Hivyo sioni vipi maji na mafuta vikachanganyika.”

“Ahaa!” Alitikisa kichwa Mtanzi. “Huoni kuwa wewe ni mgeni hapa? Umaarufu hauna, tajriba pia huna na hauna watu dhabiti wa kukupigania. Fauka ya hayo, nasikia hauna pesa tosha za kuendesha kampeni zako. Huu muungano utaweza kusuluhisha haya matatizo yote. Pia tukiungana nina uhakika asilimia mia kuwa tutashinda.”

Mariko alitikisa kichwa na kumkita Mtanzi jicho kali kisha kwa mazingatio akaanza kunena.

“Mimi nitakwamba tena. Siasa si umaarufu, si pesa au ata nguvu. Kiongozi bora hujiuza kwa sera. Mimi sina matatizo yoyote. Walio na matatizo ni wenyeji wa Takia na matatizo yenyewe yanahitaji kusuluhishwa. Ninaamini kuwa nina ufunguo wa kuwaepua wanatakia toka lindi hili la uchochole. Samahani lakini sina nia ya kukubali ombi lako.” Mariko alihitimisha.

“Doh!naona una uchu kweli. Basi mimi sina budi kukutakia mema.” Mtanzi alikubali shingo upande. 

Hata hivyo Mtanzi alimsindikiza tu kwa maneno kisha akapanga hatua nyingine ya kuchukua. Aghalabu aliazimia kung’oa magugu yote yaliyotishia kuizima choyo yake ya kutaka kuiongoza Takia. Ndani yake alidhamiria kuongoza hadi kifo kimuepue uongozini bali si binadamu kama yeye. 

Itaendelea… 

VUTA N'KUVUTE Opowieści tętniące życiem. Odkryj je teraz