* * * *
Mariko aliketi chumbani pale kwa wahaka mwingi. Alibonyeza runinga ile kuiwasha na alichokutana nacho kilimwacha kinywa wazi. Picha za nyumbani kwake zilionekana kwenye runinga. Uchafu umetapakaa kote ishara ya kuwa walioishi pale walikuwa na nyoyo nzito kiasi
cha kutofanya lolote. Mara kamera ulimulika mavazi yaliyokuwa yamelowa damu. Alipoyatazama vizuri alitanabahi kuwa ni yale aliyokuwa ameyavaa usiku uliopita. Damu ilimganda mishipani na akajipata analia kwa kite.
Picha zake zilizokuwa zimebandikwa kila mahali kwa ajili ya kampeni pia zilipitishwa moja baada ya nyingine kwenye runinga. Hatimaye alitanabahi ukweli mchungu. Takia nzima ilikuwa ikiomboleza kifo cha Mariko Sipondi.Aliyesoma ulojia yake alimtaja Mariko Sipondi kama mwanasiasa aalimu aliyekuduru kupigana na siasa dhalimu na kuleta ukombozi wa pili. Alitajwa kuwa mpigania haki ya wanyonge na wachochole lakini safari hii ikakatizwa na simjui nani. Wajibu wake mkubwa ulikuwa ni
kuwarehemu Wanatakia toka kwenye mikono au minyororo ya ukoloni mamboleo.Umati wa watu ulikuwa umehudhuria mauko yake Mariko. Mkewe hakushikika na soni ya
kuondokewa na mumewe. Mwanawe Mariko, Sudi pia alizidiwa na simanzi. Alilia machozi kopo nzima ila bado hakujua kilio kilifaa vipi msiba ule uliowakumba. Kwake aliuona kama
msiba wa kujitakia ambao katu hauambiwi pole. Kilio na majonzi yake ilichukua siku kadhaa
kumwisha moyoni. Aliona maisha kuwa hayakuwa na maana tena kwani babake ndiye
aliyekuwa wakimtegemea kwa kila kitu. Kuuka kwake kukaonekana kuwa mwisho wa kuwaka
kwa mshumaa wake wa matumaini.Jioni ile baada ya mavazi ya babake kufukiziwa mchanga na wageni kufumukana, alijitosa sebuleni na kumkuta mamake katika hali aliyotarajia, uso ukiwa umesawijika na amejikunyata kitini.
Majirani wote walikuwa wameondoka sasa walibaki na maruerue ya kuondokewa na
mwenzi wao. Alijongea taratibu hali kafumbata mikono yake miwili."Sitarudi shule tena!" aliripoti Sudi. Alisita na kutokomea kwa kilio cha kwikwi.
Siku iliyofuata ikawa kisa kingine kilichogonga vichwa vya habari ni kupotea kwa mwanawe Mariko, Sudi. Ikawa kisa baada ya mkasa. Sudi baada ya kutoroka nyumbani alitanga vichochoroni asijue hasa alikoelekea. Alitaka kwenda popote pale atakapoelekezwa na miguu yake. Atokomee mbali. Maadamu apate utulivu ambao kwa muda sasa aliukosa sana.
Njaa ilipomzidi alikaa kitako kando ya njia na kuanza kutafuna matawi ya miti mwitu. Sikwambii hata jina la mti wenyewe hakuujua. Kala tu angalau auzibe ubao uliombana kifai.
Machozi tele usoni mwake yalikuwa ishara tosha ya fundo chungu sana moyoni alilokuwa nalo na halikuwa rahisi kwake kuhimili. Alivuta taswira na kumhurumia mamake ambaye sasa kamwacha nyumbani akiwa pekee yake. Aliona kafanya kosa kubwa kumwacha upweke lakini
aliona afadhali kugura maskani yao kwani kila mara akiwa pale kumbukizi za babake zilimwandama na kumtia soni si haba.Kwake yeye uamuzi wa babake wa kujitosa katika ulingo wa siasa ulikuwa kama dhambi kubwa isiyojua msamaha.Mbona kaazimia lengo alilojua fika kuwa halikuwa rahisi kutimia? Tena katika hali ya Takia? Hata hivyo, asichojua Sudi ni kuwa mja yeyote yule anapojitosa katika
kinyanganyiro fulani basi huwa na imani ya kuibuka mshindi.

YOU ARE READING
VUTA N'KUVUTE
Mystery / ThrillerMtanzi ambaye ni Kiongozi wa Takia na mgombea kiti cha uongozi cha Takia anaonyeshwa kama kiongozi aliyejaa udhalimu, majivuno, kiburi, na ukatili. Harakati za kumng'atua uongozini zinaanza Lakini pia wale wanaopania kufanya vile haijulikani Hulka y...