Hatimaye Mtanzi alikamilisha hotuba yake iliyojaa majivuno na kujimiminia sifa sufufu. Aliketi mkabala wake Masumbufu na wakaonekana wakinong'onezana kwa furaha. Mariko alibonyeza kuizima runinga na kumkita jicho Mhazili. Akazamisha kichwa chake viganjani mwake na kuanza kulia. Pasi na shaka alihurumia Takia kwa aina ya viongozi ambao walikuwa
wanachukua usukani.Mhazili alimwonea imani Mariko sana. Akasogea na kuutia mkono wake begani mwake na akaanza kulengwalengwa na machozi. Mariko aliinua uso kumtazama na kushangaa nini kilichomwingia jamaa yule. Hata mlango wa 'gereza' lile lake Mariko alikuwa ameuacha wazi na Mariko alikuwa huru kutoka. Aliinuka na kuelekea mlangoni lakini alipokuwa amekaribia kufika, aliisikia sauti yake Mhazili ikitanda nyuma yake ikimwamrisha asichukue hatua zaidi.
"Usithubutu ikiwa bado wataka kuona familia yako." alisema akiwa ameshikilia bastola kisogoni mwake Mariko. Mariko alinywea na hapo Mhazili akaufunga mlango.
"Chukua hayo mavazi ukaoge kisha uyabadilishe. Mariko akatii na kuingia hamamuni. Akajinadhifisha kwa mara ya kwanza baada ya majuma kadhaa ya kutoona maji. Aliingia bafuni na kuoga na kisha
akavalia mavazi masafi aliyokuwa ameletewa na Mhazili.Pale sebuleni Mhazili alibaki akifikiria kuhusu mambo mengi. Alimhurumia Mariko na alitamani
kumweleza nia yake na Mtanzi. Baada ya dakika chache alitoka bafuni na mkononi amebeba mararu yale yake. Akamkabidhi Mhazili ambaye kisha aliyatia ndani ya karatasi.
Alionekana nadhifu licha ya udhaifu aliyokuwa nayo."Haya kale." Mhazili akamkabidhi kifurushi cha chakula ambacho kwa mshangao wake Mariko kilikuwa kingi na kilikuwa kimepikwa kikapikika.
"Nataka unisikilize kwa makini." Mhazili alianza baada ya kimya cha muda. "Mimi sina nia ya
kukuua kama nilivyoamrishwa na Mtanzi." Mariko akaacha kula kwanza na kumgeukia Mhazili.
Macho yake yalionyesha dhahiri shahiri aliyamaanisha matamshi yake. "Lakini fahamu kuwa
hutoiona familia yako maana Mtanzi akipata habari kuwa bado u hai basi sote tutakuwa mashakani.""Haitowezekana hivyo." Mariko alikana. "Familia yangu ilinitegemea kwa mahitaji yote ya kimsingi. Sasa naona wanateseka kwa kunikosa. Isitoshe wanatakia wanafaa kujua aina ya nduli wanaowaongoza ili waondolewe mamlakani mara moja. Ni wakati sasa wa haki kutendeka."
Mariko alikariri.
"Fahamu kuwa nayafanya kwa usalama wangu na wako. Mtanzi akija kujua hujafa kama alivyoelekeza basi ujue huo ndio utakuwa hatima yangu na yako. Siuthamini uongozi wake licha ya mimi kuwa msiri wake mkuu. Kumfanyia kazi kwa miaka hii yote haijanifaidi chochote kwani nimeishi kutenda mabaya. Nadhani laana niliowatenda umma zinanifuata na kunifanya kutofaidhika na pesa ninazochuma kwa kufanya mabaya." Baada ya kuyasema hayo
akaukomelea mlango na kutokomea.
Alitaka kuuwahi wakati kabla ya machweo. Hakusahau
kwenda na mavazi yale yake Mariko kwenda kuyatupa karibu na kituo cha polisi. Hapo akafululiza hadi nyumbani kwake.
YOU ARE READING
VUTA N'KUVUTE
Mystery / ThrillerMtanzi ambaye ni Kiongozi wa Takia na mgombea kiti cha uongozi cha Takia anaonyeshwa kama kiongozi aliyejaa udhalimu, majivuno, kiburi, na ukatili. Harakati za kumng'atua uongozini zinaanza Lakini pia wale wanaopania kufanya vile haijulikani Hulka y...