Episode 34

10 1 2
                                    

* * *
Bwana Tadi naye moyo ulimwenda kasi akifuatilia kwa karibu matukio ya uchaguzi ule. Mara mlango wake ulibishwa na ndani alijitosa Fahama Makumbo.
"Alaa! Nini la mno?" alishangaa Tadi.
"kwani hujapata habari?" Fahama alishangaa.
"Habari zipi?"
"Kuwa kuna njama za kuiba kura?!"
"Ukweli?" Tadi alisaili kwa butwaa.
"Ndiyo. Kuna madai vituo ambavyo havikusajiliwa kisheria vimeruhusiwa kupiga kura na kura
zenyewe zinaonekana kumwendea Mtanzi. Nafikiri Mtanzi mwenyewe amepanga njama hii ya kutupoka tena kura. Usikubali mara hii Tadi. Unajua huenda ikawa mara yako ya mwisho
kugombea kiti hiki na lazima upiganie haki yako. Huyu Mtanzi amezoea kuiba sana."
"Unadhani madai haya ni ya kweli?" Tadi alitathmini.
"Mbona yasiwe ya kweli wakati pia wewe wajua hulka yake Mtanzi. Si mara yake ya kwanza
kufanya hivi. Yasemwayo yapo na kama hayapo basi yaja." Fahama alisema.
"Walipo Tadi na Matata hapakosi matata. Matata mwenyewe anazo kesi nyingi zinazomkumba ilhali bado anakalia nafasi kuu ya uongozi huku Takia. Mara hii hawatoniibia tena lazima nipiganie haki yangu. Hata hivyo tungoje tuone matokeo kwanza ndipo tuweze kutoa msimamo
wetu."

Walipokuwa wanaendelea kupiga bongo kuhusu mikakati watakayochukua walisikia sauti ya
mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kwenye kipaaza sauti.

"Tuna furaha kuwa zoezi hili la
uchaguzi limefanikiwa na hatujakuwa na hitilafu yoyote wala kupokea malalamishi yoyote.
Tungependa kuwahakikishia wanatakia kuwa uchaguzi huu umekuwa wa huru na haki na
matokeo yatakayotolewa yanalingana na maazimio ya wanatakia. Tunahimiza kuwe na utulivu na amani kwani vurugu si suluhisho. Tujue kuwa kwa kila shindano kuna mshinda na mshinde."

Usemi huu ulitua masikioni mwa wagombeaji wote waliojitokeza kuchaguliwa uchaguzini. Wote
walikuwa na matumaini ya kushinda uchaguzi ule. Mhazili alishusha pumzi kwa nguvu baada ya tangazo lile. Alipiga bongo na kuamua hangeenda kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi wakati tangazo la mshindi likitolewa. Mtanzi alipompigia simu alisema kuwa alikuwa mgonjwa na hivyo hangeweza kuandamana naye.
Akilini alijua kuwa msako wa kumtafuta Mariko ungeendelea na alitaka uwe wazi kuwa kutafuta
huko ni kupoteza wakati. Alitaka pia kitu ambacho kingemfanya Mtanzi aamini kuwa Mariko alikuwa marehemu.

Alivalia kabuti lake na kama kawaida akaenda kuazima gari lake Mambo. Alitaka kumdanganya kuwa anaelekea kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi kama njia ya kumfanya Mambo kumwamini.

Mhazili alitia gari moto na kuelekea eneo la Matambiko alipokuwa amemchukua Mariko mateka. Alimpata Mariko akiwa anakoroma. Alikuwa hajaamka tangu pale alipochukuliwa na usingizi mzito.Akizinduka pale aliposikia mlango ukifunguliwa. Aidha nderemo kutoka runingani ilizidisha kelele na akazinduka. Aliamka haraka na kuyapangusa macho yake.
Akayakodolea runinga. Mtanzi alikuwa ametangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Takia.
Pia Mhazili alijitosa ndani na kuyakodolea macho matukio yaliyokuwa yakiendelea. Ni kama
hakuamini kile alichokuwa anakiona. Mariko alitazama uso wake Mhazili na kushangaa kwa nini
alionekana kutoridhika na ushindi wake. 'Ama si kibaraka wake Mtanzi?' Mariko alijisaili.

"Ningependa Mtanzi, ambaye ndiye kiongozi wetu mteule ahutubu tu kwa ufupi." Sauti yake mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ilisema.

Mtanzi akaitwaa kipaaza sauti ile kwa madaha na akajaza tabasamu nzito usoni. Bwana Matata Masumbufu naye hakusita kuweka tabasamu
ulioonyesha meno yake yaliyogeuka rangi sababu ya uraibu wa kutumia mihadarati.

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now