VUTA N'KUVUTE
Inaendelea...
"Usithubutu kupiga ukemi ikiwa bado unayathamini maisha yako." Sauti ya Mhazili ilitanda gizani. Mariko akatii bila neno. Macho yake yalimtazama kwa kina jamaa huyu ambaye sasa alikuwa ashavua barakoa yake na kuitia mfukoni. Alimtia Mariko pingu na kumburura katikati ya msitu wa Tuungane. Mara walitokea eneo lililokuwa wazi ambapo Mhazili alikuwa ameliegesha gari alilokabidhiwa kwa ajili ya kazi ile. Mariko akashindiliwa ndani ya buti mithili ya gunia la viazi. Mhazili akalitia gari moto na kuliondoa kasi. Mariko hakuwa na habari ni wapi alikuwa akipelekwa.
Mariko alisafirishwa msituni kwa muda mrefu. Licha ya kuwa mwenyeji wa Tuungane, Mariko hakuwahi kutalii msitu na kuujua asili na fasili yake. Hatimaye gari lilisimama na akabururwa na kufungiwa ndani ya gofu moja la nyumba ambalo lilitishia kumporomokea wakati wowote.
Mhazili aliketi mbele yake Mariko na kumtazama kwa muda na kisha akatoka. Muda mfupi akarejea na kifurushi cha chakula na kumkabidhi Mariko ila alidinda hata kukionja. Licha ya juhudi zake Mhazili kumrai ale, aliambulia patupu. Hapo Mhazili akatoka na kuelekea nyumbani kwa Katu.
Kwa upande mwingine, Sumeha alikuwa tayari amepatwa na kihoro sababu ya kuchelewa kwa mumewe. Kila mara alitazama saa yake na kuchungulia kwa matumaini ya kumwona lakini wapi. Kadri muda ulivyosonga ndivyo uwoga ulivyomkaba zaidi. Haikuwa laiki ya Mariko kuchelewa kufika nyumbani na ikiwa angechelewa huwa anamwarifu mkewe. Ila leo mambo yalikuwa tofauti.
Itaendelea...

YOU ARE READING
VUTA N'KUVUTE
Mystery / ThrillerMtanzi ambaye ni Kiongozi wa Takia na mgombea kiti cha uongozi cha Takia anaonyeshwa kama kiongozi aliyejaa udhalimu, majivuno, kiburi, na ukatili. Harakati za kumng'atua uongozini zinaanza Lakini pia wale wanaopania kufanya vile haijulikani Hulka y...