Episode 28

17 3 2
                                    

Licha ya kazi aliyomfanyia Mtanzi kwa miaka mingi, Mhazili hakuwa amefaidika sana. Hakuwahi
kupata zawadi kubwa na ambayo angejivunia. Hata hivyo hakuwa na lingine kwani hali ya
umaskini ya Takia haikumpa fikira za kutaka kuacha kazi ile. Sasa aliganda tu pale muradi apate
cha kujikimu yeye.
Punde tu alipotoka kwa Mtanzi, aliamua kwenda pale alipokuwa amemficha Mariko maana alijua
kuwa pindi msako utakapofikia kilele huenda akapatikana. Hata hivyo hakuwa na motokaa
ambayo angeitumia kufika msituni Tuungane. Akapiga bongo na hatimaye akamkumbuka jirani
yake aliyekuwa na teksi aliyofanya nayo biashara.
Alipofika kwa Bwana Mambo, alimkuta tayari ashatoka kazini kwani ilikuwa ni wakati wa jioni.

"Safari ya wapi saa hizi?" Mambo alimuuliza.
"Hapa tu kwa Mtanzi. Niliona imekuwa jioni sana na saa hizi kupata magari ya umma ni
ngumu." Mhazili alidanganya.
"Huyu Mtanzi unayemfanyia kazi hukulipa pesa ngapi? Mbona asikununulie gari na
unavyomfanyia kazi kwa bidii?" Mambo alijawa maswali.
Mhazili mwanzo alipatwa na kitata huku akifikiria. "Si wewe wamjua Mtanzi vizuri? Ni
kigeugeu mkuu." Mhazili alijibu.
"Basi si lazima umfanyie kazi kama huoni faida yoyote. Mbona ufanye kazi isiyokufaidi?"
Hayo tutayazungumza baadaye kwa sasa nahitaji kufika huko haraka.' Mambo akamwazima
Mhazili gari lake. Mhazili alifanya hima kwani saa zilienda kasi na alitaka kumhamisha Mariko
kabla hajapatikana na watafutaji. Aliongeza kasi na muda si muda, alikuwa msituni Tuungane.
Aliegesha gari kando ya msitu ule na kutembea kwa miguu maana gari lile halingepenya msitu ule.

Mariko alikuwa amejikunyata pale alipokuwa amefungiwa. Njaa kali ilimwumiza kwani alikuwa
hajala tangu alipotekwa nyara. Alimtazama Mhazili kwa kina. Alikuwa hajawahi kumwona
popote pale. Hata hivyo aliona kuwa wanashabihiana sana na Mhazili, msiri wake Mtanzi.
Mawazo yake mara yalianza kufikiria hali ya familia yake. Alimhurumia mkewe kwani alijua
hakuwa akipata lepe la usingizi kwa sababu ya simanzi. Alimhurumia mwanawe ambaye
alikuwa amesikitikia uamuzi wake wa kujiunga na siasa. Alijihurumia kwa hali aliyokuwa akijua
fika kuwa hangepata usaidizi wowote. Si kwa sababu hakukuwa na uwezo wa kumpata ila kwa
sababu watu wachache hawangetaka apatikane na wangefanya kila juhudi kuhakikisha hilo.
Fikira tumbi nzima hazikusita akilini mwake. Alijiuliza ni kwa nini kiongozi aali kama yeye
alipitia dhuluma kama hizo. Ama ni kweli kuwa waliojaribu kuleta unadhifu wa kisiasa mjini
Takia walifagiliwa?
Ghafla fikira zake zilitia nanga pale aliposikia mchakato wa matawi kwa umbali. Mwishowe
Mhazili alijitosa ndani ya gofu lile alilokuwa amefungiwa Mariko akiwa ameshikilia kurunzi
yake mkononi. Kurunzi ile ilitoa mwanga uliomulika kila kilichokuwa pale ndani. Mariko
alifumba macho maana mwanga ule ulikuwa mkali sana. Alifakamia kwa pupa chakula
alichokuwa ameletewa na Mhazili kwani alikuwa amebanwa na ubao kifai.
"Hamna wakati wa kupoteza. Tunaondoka." Mhazili alikata kimya kilichokuwa kimejiri baina
yao.
"Tunaenda wapi?" Mariko aliuliza kwa unyonge.
"Msitu huu ni hatari kwa usalama wako. Hapa wahuni ni wengi na pia wanyamapori kali wapo.
Nakupeleka pahali palipo salama."
"Kwa nini uko na haja na usalama wangu wakati nia yako ni kuniulia mbali? Mniue ndipo mpate
faida zipi? Kubakia mamlakani na kuendelea kupora mali ya Takia? "
"Nyamaza!" sauti yake Mhazili ilitanda. "Mimi nafuata tu masharti."
"Kutoka kwa nani?'

Utafahamu hivi karibuni. Kilicho muhimu kwa sasa ni tufike tunakokwenda." Mhazili alinena.
"Mnataka kuniua ili msije mkang'atuliwa mamlakani na maovu yote mliyotenda miaka hii yote
ikafichuka. Hata hivyo kifo changu hakitakuwa mwisho wa ndoto hii ya kutaka kuikwamua
Takia toka mikononi mwa wakoloni weusi. Msije mkadhani mtabaki uongozini daima. Leo
huenda ni siku yangu ya kufa lakini kumbuka kifo hujia wote."

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now