Inaendelea…
Mhazili alifika Tuungane mapema kiasi cha haja. Hakuandamana na yeyote yule licha ya kuagizwa kutafuta vijana wa kazi. Alirandaranda huku na kule akiangaza macho kuwatazama wanabiashara waliokuwa katika harakati za kufunganya tayari kuondoka.
Giza lilianza kuingia taratibu kijijini Tuungane na mji wa Takia kwa ujumla. Wenyeji wa Tuungane walianza kufanya halahala ili kuwahi makao yao kabla ya giza kuigubika eneo lile. Mhazili naye alizidi kutalii akingojea wakati mwafaka kutenda alilojia. Alijua fika saa za Mariko za kurudi nyumbani toka kazini kwani Katu alikuwa amempa habari zote. Hakutaka kumkosa.
Palipoonekana shwari, Mhazili alijibanza kando ya njia ndani ya kichaka kikubwa ambacho kilimsitiri vizuri. Alitwaa barakoa aliyokuwa nayo mfukoni na kisu akakiweka sambamba. Akangoja kwa hamu na wasiwasi pia.
Wakati huo Mariko alijikokota taratibu huku akitembea kwa kasi kabla achelewe zaidi. Alivuta taswira ya jinsi mambo yalivyokuwa na yatakavyokuwa pindi tu yeye atakapotwaa kiti cha uongozi. Alikuwa na imani kuwa katu hatageuka imani ya wanatakia akiingia mamlakani.
Siku tatu uchaguzi ulijongea kasi na Mariko alikuwa na imani kuwa atatwaa mamlaka na kuisafisha Takia. Aliamini kuwa atairejesha Takia katika orodha ya miji tajika. Aifanye iwe mji wa kujivunia na watu wake. Sasa alikuwa na ufuasi mkubwa na sera zake zenye mashiko zilizungumziwa kote.
Katika harakati za kupanga na kupangua kimawazo, ghafla alikabwa koo asiweze hata kpumua au kupiga ukemi. Kisu kilichonyota gizani kilitiwa shingoni mwake. Lo! Uwoga ulimzizima Mariko na moyo kumwenda kasi.
Itaendelea…
KAMU SEDANG MEMBACA
VUTA N'KUVUTE
Misteri / ThrillerMtanzi ambaye ni Kiongozi wa Takia na mgombea kiti cha uongozi cha Takia anaonyeshwa kama kiongozi aliyejaa udhalimu, majivuno, kiburi, na ukatili. Harakati za kumng'atua uongozini zinaanza Lakini pia wale wanaopania kufanya vile haijulikani Hulka y...