Inaendelea…
Sasa miaka ishirini ilikuwa imepita tangu wao kupokwa shamba lao. Ila aliyetenda kitendo hicho akibakia kitendawili kisichoteguka. Fikira hizi zilimfanya Bi. Mterehemezi kububujikwa machozi kupukupu. Kilio chake kikamzindua Tadi kutoka usingizini.
Mteheremezi aligutuka na kufuta machozi haraka. Hatimaye waliruhusiwa kuondoka hospitalini. Wakashika njia kuelekea nyumbani kwao. Dereva wao alikuwa tayari anawasubiri nje ya hospitali ile. Wakaingia garini na kuondoka.
Baada ya kimya cha muda mrefu Tadi aliamua kukivunja kimya kile.
“Yule Mariko alikuwa na nia gani?” Tadi alisaili.
“Hakuwa na nia mbaya, nafikiri alikuwa amekuja tu kusikiza.” Mterehemezi alijibu.
“Hamna! Huoni alivyovuruga hadhara yangu? alifoka Tadi.
“Nawe ukaona ulipishe moto kwa moto?” Mterehemezi alizidi kuchochea.
“Alistahili.”
“Alistahili!?” Alishtuka Mterehemezi. “Huoni wanamji wasio na hatia walivyoumia? Walikuwa na hatia gani wale watu waliokuwa mkutanoni?”
Tadi hakujibu. Alimkita mkewe jicho kali na kuendelea kufikiria. Hakujali. Maadamu fahali wawili wapiganapo nyasi ndizo huumia.
“Yule ni nduli. Ni hatari kwa amani ya Takia. Hafai kuchochea umma kuzua rabsha.”
“Hakuzua rabsha yoyote. Sera zake ndizo zafurahisha wanatakia.”
Kauli hii ilimfanya Tadi kumtupia mkewe jicho la uhasama. Uhasama ambao kwa miaka na mikaka ulijikita na kujisitiri ndani ya moyo wake Tadi. Laiti Mterehemezi angefahamu hulka ya Tadi, asingekuwa mkewe.
“Wamaanisha nini?” Alikuja juu Tadi. “Kuwa mimi sina sera?”
“Katu simaanishi vile. Ila wewe una sera kwa maneno tu si kwa vitendo. Jiulize, ni mara ngapi umejaribu kupigania uongozi wa mji huu na kila uchaguzi unapokamilika unaambulia patupu? Hujaelewa nini sababu ya kuanguka kwako? Sera zikiwa maneno matupu haziwezi kusaidia. Sera hufuatwa na vitendo.” Mterehemezi alilimwaga dukuduku lake lote.
Itaendelea…
YOU ARE READING
VUTA N'KUVUTE
Mystery / ThrillerMtanzi ambaye ni Kiongozi wa Takia na mgombea kiti cha uongozi cha Takia anaonyeshwa kama kiongozi aliyejaa udhalimu, majivuno, kiburi, na ukatili. Harakati za kumng'atua uongozini zinaanza Lakini pia wale wanaopania kufanya vile haijulikani Hulka y...