Episode 37

8 0 0
                                    

Mtanzi na Masumbufu waliketi nje ya ofisi yao wakipunga hewa. Wakati huo walikuwa wakisubiri tu kuapishwa kwao ili kuanza kazi mara moja.

"Huyu Mhazili kaadimika sana siku hizi. " Masumbufu alianza.

"Hata mimi nina wasiwasi naye. Ukiona mtu anajaribu kukuhepa namna anavyofanya Mhazili ni ishara tosha kuwa huenda ana mipango mingine ama amepata kazi nyingine nzuri." Mtanzi alisema.

"Alaa! Kuna kazi gani nyingine nzuri kuliko kumtumikia kiongozi wa mji kama Takia? Mtu kama huyo basi ni juju asiye na mfano." Masumbufu alisema huku akiangua kicheko kikuu.

Soga ilivyozidi kunogea, Mhazili alionekana kwa mbali akikaribia. Mkononi alikuwa amebeba
gazeti la siku hiyo. Akakaza mwendo na alipowaona Mtanzi na Masumbufu wakiwa wameketi nje, akajitia bashasha usoni. Masumbufu alimtazama kwa macho kaguzi bila kusema lolote. Mhazili na Mtanzi wakabaki wakikumbatiana kwa furaha kuu.

"Asante sana kwa kufika. Umepotea sana." Mtanzi alinadi kwa furaha tele.

"Shughuli ni nyingi lakini kilicho muhimu ni kuwa sasa nipo hapa kukutumikia." Mhazili aliyasema hayo huku akimkabidhi Mtanzi nakala ya gazeti lile. Aliyasoma maandishi makubwa ya kichwa cha gazeti lile na na kutabasamu. Lilisoma hivi: NGUO ZA MARIKO ZAPATIKANA BILA MAITI

Mtanzi akaangua kicheko kikubwa cha kutisha na kumkabidhi Masumbufu nakala yenyewe.

Masumbufu akapokea kwa pupa maana kicheko chake Mtanzi kilimtia hamu ya kutaka kujua

kikichomchekesha mwenzake. Pia yeye alionekana kutabasamu na kisha kumtazama Mtanzi.

"Sasa waona, mpiga ngumi ukuta huumiza mkono wake." Masumbufu alikaulisha.

"Pasi na shaka. Alidhani kuwa ana nguvu ya kutung'atua uongozini lakini hakujua kuwa vita hivi

tumepigana kwa muda mrefu. Sasa amefahamu kuwa wavumao baharini ni papa." Mtanzi alitilia pondo.

"Hivi karibuni haya yote yatasahaulika kama kwamba

hayakutendeka." Mhazili alimalizia.

"Vizuri kabisa. Naona ninao watu wanaofahamu fika kazi zao. Wewe na Katu mtapata mgao mwingine wa pesa kama shukrani kwa kazi nzuri." Mtanzi alinena. Mhazili akamshukuru na kuondoka huku Mtanzi na Masumbufu wakibaki kusherehekea 'kifo' cha Mariko.

VUTA N'KUVUTE Where stories live. Discover now